Meya aahidi kujenga kiwanda cha mbolea

28Dec 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Meya aahidi kujenga kiwanda cha mbolea

SERA ya Rais John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda ili kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, ‘umemkuna’ Meya wa Manispaa ya Moshi Raymond Mboya (Chadema), ambaye ameahidi watamuunga mkono kwa juhudi zake mwezi Februari, mwakani kujenga kiwanda cha kutengeneza mbolea.

Kiwanda hicho kitajengwa kwa ubia kati ya Manispaa ya Moshi na Mji dada wa Tübingen wa Germany, karibu na dampo kuu la Manispaa hiyo lililopo eneo la Kaloleni.

Alitangaza ahadi hiyo jana, wakati akitoa ripoti yake kwa umma kuhusu kazi za maendeleo zilizofanyika mwaka 2017 na zitakazoanza kutekelezwa mapema mwaka ujao.

“Tunamuunga mkono Rais (Magufuli) katika suala la ujenzi wa viwanda na kweli juhudi zake zimetupendeza na tumeamua tutamuunga mkono mwezi Februari mwaka 2018, kwa kujenga kiwanda kipya cha kutengeneza mbolea eneo la Kaloleni…Tunasubiri barua rasmi ya uwekezaji wa mradi huo kutoka kwa wenzetu ambao ni mji dada wa Tübingen,” alisema.

Katika taarifa yake, Meya huyo alisema mwezi Januari, mwakani, Tubingen na Manispaa ya Moshi, watasaini makubaliano ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachotarajiwa kutumia malighafi ambayo ni takataka zinazokusanywa katika Manispaa ya Moshi.

Alisema kwa sasa wanajiandaa kwenda kutoa taarifa na kutambulisha mradi huo kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.

Kwa mujibu wa Raymond, kila siku mji wa Moshi unazalisha taka, kati ya tani 180 hadi 200 na kwamba timu ya wataalamu wa ujenzi wa kiwanda hicho kutoka nchini Ujerumani, wameshakuja na kufanya tathmini na kujiridhisha malighafi hiyo inaweza kuendesha uzalishaji wa mbolea.

Ujenzi wa kiwanda hicho, unatokana na kukosekana kwa teknolojia ya kubadili taka ngumu zinazozalishwa na wakazi wa Manispaa ya Moshi ili zitumike kama nishati.

 

Habari Kubwa