Mamilioni yamwagwa miradi uchumi vijana

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Mamilioni yamwagwa miradi uchumi vijana

KATIKA kuchangia juhudi za serikali kuelekea uchumi wa kati wa viwanda, Taasisi ya An Naal imetoa zaidi ya Sh. milioni 500 kwa ajili ya mafunzo na uanzishaji miradi ya kiuchumi kwa vijana 50 nchini.

Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam katika ufungaji wa mpango huo wa miaka miwili, Mkurugenzi Miradi wa taasisi hiyo, Musa Ally, alisema katika kipindi hicho vijana walijifunza njia ya kuibua mawazo, matumizi sahihi ya fedha na uendeshaji miradi kwa manufaa ya jamii.

Alisema fedha hizo zimetolewa kwa ufadhili ya Mfuko wa Fedha wa Nama kutoka nchini Indonesia.Alisema malengo makuu ya mpango huo ni kuwajenga vijana kuwa na moyo wa kujitolea na kusaidia jamii kutokana na uwezo wao.

“Taifa linahitaji vijana wabunifu, wenye dira ya kimaendeleo na wanaoguswa na matatizo ya watu masikini. Mpango huu unalenga kuwaondoa katika mawazo hasi ili kuona wana wajibu wa kutatua wao kwanza kabla ya serikali,” alisema Ally.

Hata hivyo, vijana wanne walipewa zaidi ya  Sh. milioni 9.3 kama mitaji  baada ya miradi yao kuibuka na ushindi.Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nama, Saleh Bazaed, alisema taasisi yake imeamua kufadhili mpango huo baada ya kuona kuna umuhimu kwa vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu maendeleo ya nchi yao.

Alisema ni muhimu kuwekeza kwa vijana katika elimu ya ujasiriamali kutokana na kundi hilo kuwa na nguvu kubwa ya kiakili, kimbinu na kimaamuzi.

“Tumefadhili mpango huu tukiamini kwamba vijana hawa wataweza kupeleka mwamko mpya huko wanapokwenda na hatmae kusaidia nchi yao na jamii kwa ujumla,” alisisitiza Bazaed.

Mmoja wa washindi hao, Abdallah Ndale, alisema wanazishukuru taasisi za An Naal na Nama kwa kuwawezesha elimu na mitaji na kwamba watakaporudi katika jamii zao wataanzisha miradi ambayo itawagusa moja kwa moja. 

Habari Kubwa