Makalla aonya maofisa mifugo dhidi ya rushwa

16Jul 2017
Nebart Msokwa
Nipashe Jumapili
Makalla aonya maofisa mifugo dhidi ya rushwa

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, amewatahadharisha maofisa mifugo katika Wilaya za Chunya na Mbarali mkoani humo kuepuka vitendo vya rushwa wakati wa kutekeleza agizo la Serikali la kusajili na kuipiga chapa mifugo ili kuepuka kuzalisha migogoro.

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla.

Makalla alitoa tahadhari hiyo juzi wakati akizindua zoezi la kupiga chapa mifugo katika Wilaya ya Mbarali ambalo lilifanyika katika Kijiji cha Azimio Mapula ambapo alisema lengo la Serikali ni kutaka kuweka utaratibu mzuri wa ufugaji.

Alisema maofisa mifugo wanaweza kuanza kuitumia fursa hiyo kupokea rushwa kwa wafugaji wa mikoa mingine ili waje wasajili mifugo yao kwenye wilaya hizo jambo ambalo alitahadharisha kuwa ikibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Vilevile alisema watumishi hao wanaweza wakawa wanapokea rushwa kwa wafugaji waliosajiriwa ili wafiche baadhi ya mifugo bila kuisajili na kupigwa chapa na kwamba watakuwa wanajidanganya bure kwani kutakuwa na ufuatiliaji.

“Tunataka mifugo yote isajiliwe na ipigwe chapa ili tunapopanga bajeti ziwe na uhalisia, tunataka kupunguza wizi wa mifugo, migogoro ya wakulima na wafugaji na kuweka matumizi bora ya ardhi, sasa kuna baadhi ya maofisa mifugo wanaweza wakalinajisi zoezi hili kwa rushwa, sasa nawatahadharisha wasithubutu,” alisema Makalla.

Hata hivyo, aliwaagiza wakuu wa Wilaya hizo kuteua baadhi ya maofisa kutoka kwenye idara zingine ili washirikiane na maofisa hao kuhakikisha zoezi hilo linafanyika bila kikwazo.

Akizungumzia maandalizi ya zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, alisema yeye mwenyewe kwa kushirikiana na watendaji mbalimbali wa Ofisi yake, wamefanya mikutano mbalimbali na wafugaji katika Wilaya hiyo kwa ajili ya kuwaelimisha umuhimu wa zoezi hilo.

Alisema wengi wao walikubali na kuonyesha mwitikio mkubwa na kwamba kwa sasa wanaendelea kuhamasisha katika kata chache ambazo zilikuwa bado wakati wataalamu wakiendelea kupiga chapa kwenye kata ambazo uhamasishaji ulishafanyika.

Alisema zoezi hilo kwa Wilaya yake litasaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa kero katika miaka ya hivi karibuni kutokana na uingizwaji wa mifugo kinyemela kutoka katika Wilaya zingine.

Vilevile, alisema zoezi hilo litasaidia kupunguza migogoro kati ya wafugaji na Mamlaka ya Hifadhi za wanyamapori (Tanapa) hasa katika Hifadhi ya Wanyamapori ya Ruaha ambayo mara kwa mara imekuwa ikivamiwa na wafugaji.

“Maagizo yote tuliyoagizwa na Mkuu wa Mkoa tutayatekeleza kwa kuzingatia sheria na tayari tulishaanza kuhamasisha na kuwaelimisha wafugaji umuhimu wa zoezi, sasa tutaendelea katika Kata chache zilizobakia ili kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza,” alisema Mfune.

Akitoa taarifa ya mifugo katika Wilaya ya Mbarali, Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya hiyo, Augustino Alawi, alisema Wilaya hiyo ina jumla ya mifugo 197,000 huku wafugaji wakiwa 7000.

Alisema zoezi hilo litakamilika ndani ya muda uliopangwa na Mkuu wa Mkoa kwa maelezo kuwa wataalamu wote watakaoshiriki kwenye zoezi hilo wameshaandaliwa.

 
 
 

Habari Kubwa