Majaliwa apigia debe fursa za utajiri zao la korosho

03Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Majaliwa apigia debe fursa za utajiri zao la korosho

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaoishi kwenye mikoa ambayo zao la korosho linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo kwa sababu lina fursa nyingi.

“Mahitaji ya korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika hotelini na kwenye mikutano mikubwa, zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe kubwa,” alisema.

 

Alisema hayo, wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi.

 

Alisema anaamini kijana yeyote mwenye nguvu ya kufanya kazi hawezi kushindwa kulima zao hilo kwa sababu halihitaji uangalizi mkubwa. “Kijana yeyote anaweza kulima zao hili kwa sababu ekari moja ina miche 37 hadi 40. Kuna mtu atashindwa kuangalia miche 37 hadi ikue?” Aliuliza.

 

Alisema kilimo cha korosho ni rahisi, lakini ni rafiki wa mazingira, kwani miti ikikuwa inatunza mazingira na inasaidia kuleta mvua. Alisema mbali ya mikoa inayolima korosho ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga, kuna mikoa mingine ambayo udongo wake umepimwa na kubainika zao hilo linaweza kustawi bila shida.

 

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe, Songwe na kuongeza kuwa mikoa ya Singida na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi wake.

 

Akitoa taarifa ya uzalishaji wa miche ya mikorosho msimu wa 2017/18 mkoani Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Ramadhani Kaswa, alisema katika msimu wa 2016/2017, mkoa huo uliweka lengo la kuzalisha na kupanda miche 1,000,000 ya mikorosho.

 

“Hadi mwisho wa msimu huu, jumla ya miche 716,532 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima sawa na asilimia 71.6 ya lengo lililowekwa. Kati ya hiyo, Halmashauri ya Kilwa ilizalisha miche 55,000, Halmashauri ya Lindi miche 100,000, Manispaa ya Lindi miche 50,000; Halmashauri ya Liwale miche 106,000; Halmashauri ya Nachingwea miche 227,670 na halmashauri ya Ruangwa miche 177,862,” alisema.

 

“Miche hii iligawanywa kwa wakulima bure ambao walipanda kwenye mashamba yao. Zoezi la tathmini ya miche iliyokua baada ya kupandwa linaendelea kwenye halmashauri zote za mkoa,” aliongeza.

 

Kaswa alisema kutofikiwa kwa lengo hilo kumechangiwa na kutopatikana kwa mahitaji yote ya mbegu na vifaa vya uzalishaji, kuchelewa kwa vifaa, na mwamko mdogo wa vikundi vya uzalishaji.

Habari Kubwa