Kisa bosi CRDB kung’atuka 

29Dec 2017
Salome Kitomari
Nipashe
Kisa bosi CRDB kung’atuka 

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei, ametangaza kuachia nafasi hiyo ifikapo 2019 baada ya kuongoza taasisi hiyo kwa miaka 20 akisema inatosha. 

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, akizungumza na waandishi wa habari juu ya mchakato wa kumpata mrithi wake baada ya kustaafu mwaka 2019. Kulia ni Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Tully Mwambapa na Mkurugenzi wa Mikopo, James Mabula. PICHA: SELEMANI MPOCHI

Kutokana na kutangaza kung’atuka, amesema anaruhusu mchakato wa miezi 18 kumpata mrithi wake.

Dk. Kimei alitangaza uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari huku akieleza mafanikio makubwa yaliyopatikana miaka 20 aliyokuwa kiongozi wa benki hiyo. 

“Nimeongoza benki kwa miaka 20. Nafikiri ni wakati mwafaka kumwachia mtu mwingine naye aendeleze nilikoishia au zaidi. Nimetangaza mapema ili kuruhusu mchakato wa kupata mrithi ambao huchukua muda mrefu.

Huwezi kuongoza siku zote, lazima uachie wengine, hivyo nimeona umuhimu wa kufanya hivyo ndiyo maana sitaongeza mkataba,” alisema.

Ili kufanikisha mchakato huo, Dk. Kimei alisema Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo imeunda kamati maalum itakayoratibu mchakato huo utakaoanza mapema mwakani na kukamilika Januari 2019.

“Kwangu imekuwa heshima kubwa kuitumikia benki katika nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji toka mwaka 1998. Nina furaha kuona sasa imefika wakati kumwachia mtu mwingine kijiti hiki,” alisema.

Dk. Kimei ambaye anajivunia mafanikio ya benki kuwa na matawi 262 nchini na njia mbadala ya kielektroniki za kutuma na kupokea fedha zaidi ya 3,000, alisema ataendelea kuwapo kwa ili kuhakikisha anayepatikana anaendana na utamaduni wa benki hiyo.

“Najivunia mafanikio tokea nilipojiunga mwaka 1998, benki imeimarika sana. Tumekuwa kinara katika ubunifu wa bidhaa na huduma katika soko pamoja na kuifanya kuwa benki chaguo kwa Watanzania,” alibainisha.

Mafanikio mengine, alisema ni kuwaka misingi imara ndani ya benki, ambayo imewatofautisha wafanyakazi wa benki hiyo na taasisi zingine kwa kuzingatia weledi, mahitaji ya wateja kwanza, kuongeza ubunifu, uaminifu kila wakati na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Nina hakika hata nikiondoka leo, benki itaendelea kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu na kuendeleza ahadi ya benki inayomsikiliza mteja,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Dk. Kimei, Watanzania wenye sifa wanakaribishwa kuomba nafasi hiyo na kwamba kampuni ya mtaalamu mshauri itaongoza mchakato huo hadi kupata majina ya wenye sifa ambayo yatapelekwa kwenye bodi.

“Ningeweza kuondoka kimya kimya, lakini kwa utaratibu wa benki yetu katika kumpata mkurugenzi, wateja wangeshtuka kuona matangazo ya kutafuta mrithi isingeleta picha nzuri. Nimeamua mwenyewe kutokuongeza mkataba wangu utakapoisha. Nafikiri nitakwenda kufanya kazi nje ya nchi,” alisema Kimei ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Benki Tanzania (TBA).

Dk. Kimei ni mchumi mbobezi mwenye shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Uppsala,  Sweden.

Amefanya kazi katika sekta ya fedha kwa miongo mitatu, kuanzia nafasi ya Mkurugenzi wa Sera na Ukaguzi wa Benki ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB.

Mafanikio ya uongozi wake ni pamoja na kukua kwa faida kutoka hasara ya Sh. bilioni mbili mwaka 1998 hadi faida ya Sh. bilioni 108 mwaka 2016, huku rasilimali za benki zikikua kutoka Sh. bilioni 54 hadi bilioni 5.3 mwaka 2016.

Chini ya uongozi wake, CRDB imepanua mtandao wa matawi kutoka 19 mwaka 1998 hadi 262 mwaka 2017. Pia amepata tunzo mbalimbali zikiwamo za umahiri wa nyakati zote kutoka jarida la Bankers Africa mwaka 2016 na tuzo ya kiongozi bora wa mwaka. 

Habari Kubwa