Kilombero wapigwa marufuku uuzaji holela chakula

12Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Kilombero wapigwa marufuku uuzaji holela chakula

SERIKALI wilayani Kilombero, imepiga marufuku uuzwaji holela wa chakula kufuatia baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo kukumbwa na ukame na wakazi wake kuwa na tishio la kupatwa na njaa.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, James Ihunyo, wakati akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mang’ula, alisema yoyote atakayebainika kuuza nafaka wakati hana akiba ya chakula atachukuliwa hatua kali.

Alisema kuwa yapo baadhi ya maeneo tayari yameonekana yana upungufu wa chakula kutokana na ukame, hivyo ni muhimu wananchi hao wakahifadhi chakula walichanacho wakati wakiendelea na matayarisho ya mashamba.

Katika hatua nyingine, wananchi wa Kata ya Mkambarani wilayani Morogoro, mkoani hapo wanalazimika kula mlo mmoja kwa siku kufuatia mazao yao kukauka mashambani kutokana na ukame na hivyo kuiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia namna ya kuwasaidia chakula.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Juma Abdalah, alisema ukame umekuwa tishio kwao kutokana na kuotesha mbegu mashambani na kushindwa kuota huku wengine mazao yao yakikauka shambani kutokana na ukame na hivyo kuwasababishia hasara.

Aidha, aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, kitengo cha maafa kufanya jitihada za kuwasaidia chakula cha msaada kwa kuwa hali ya wananchi ni mbaya na hawana njia nyingine ya kupata chakula.

Diwani wa kata hiyo, Mohamed Mzee, alikiri kuwapo na changamoto hiyo ya wananchi hao kuwa na upungufu wa chakula na kwa sasa hawana njia nyingine ya kujipatia chakula hivyo wanahitaji msaada.

Aliwataka wananchi wanaishi eneo la Mkono wa Mara ndiyo walio na changamoto kubwa ya kukosa chakula kwa kuwa wengi wao walipanda mazao yao na kukauka mashambani kutokana na ukame.

Aidha, aliiomba serikali kuwasaidia wananchi hao kwa kuwaletea chakula cha msaada na mbegu za msaada ili waweze kuotesha katika msimu huo wa kilimo.

Alisema mbali na changamoto hiyo, bado wafugaji wanaingiza mifugo mashambani na tayari umewekwa mkakati maalumu kupitia kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, kuhakikisha wafugaji wote wavamizi wanaondolewa ili kupunguza migogoro dhidi ya wakulima na wafugaji.

Habari Kubwa