Fedha alizozuia mkurugenzi  sasa zapaua jengo la shule

01Jan 2018
Halima Ikunji
Nipashe
Fedha alizozuia mkurugenzi  sasa zapaua jengo la shule

WANANCHI wa Kijiji cha Matagata, Kata ya Kipili wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Simon Ngatunga kwa kupaua shule ya msingi kwa Sh. milioni tano alizoziokoa kwa kuzuia ziara za madiwani kutembelea Hifadhi ya Wanyama Koga.

Wakizungumza mbele ya mkurugenzi huyo jana, walisema shule ya kijiji chao hicho ilikuwa ina miaka saba bila kuezekwa kwa majengo yao, huku watoto wao wakilazimika kusoma kwenye madarasa yaliyo wazi juu na kutosoma kipindi cha masika.

Akiwakilisha wanakijiji wenzake, Bertha Edward alisema Shule ya Msingi ya Matagata ina vyumba vya madarasa viwili na ofisi moja ya walimu, huku wanaendelea na ujenzi wa vyoo vyenye matundu manane.

“Mkurugenzi tunampongeza kwa jitihada zake na kutekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli kutuletea maendeleo ya shule katika kata yetu ya Matagata," alisema Bertha.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Amina Mustafa alisema kukamilika kwa shule hiyo ni faraja kwao kwa kuwa hawakuwa na uwezo wa kununua mabati yote ya kuezeka vyumba vya madarasa.

Wanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo Dora Festo (12) na Sado Sangula (14) walisema sasa wanafurahia kusoma kwenye madarasa yaliyoezekwa na watasoma kwa bidii zaidi bila hofu ya kunyeshewa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mtendaji wa halmashauri hiyo, Ngatunga alimpongeza mwenyekiti, mtendaji na mratibu elimu wa kata hiyo kwa kusimamia vizuri fedha zilizotolewa na halmashauri hiyo, Sh. milioni tano na kufanikisha kuezekwa kwa shule hiyo na mahitaji mengine.

Ngatunga alisema halmashauri imejipanga kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Rais Magufuli ya 'Hapa Kazi Tu' kwa kuhakikisha wanatatua kero zote zilizoko katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya na maji.

Mkurugenzi huyo Ngatunga alisema kuwa fedha iliyotumika kuezeka shule hiyo ilikuwa imetengwa kwa ajili ya ziara ya madiwani kwenda kutembelea hifadhi ya wanyama Koga ili kujifunza mambo mbalimbali, lakini aliamua kusitisha ziara hiyo ili kumaliza kero ya shule hiyo kwanza.

Ngatunga alisema alikataa mapendekezo ya madiwani kutumia fedha hizo na kuamua zitumike kwa maendeleo ya shule hiyo ambayo wanafunzi walikuwa wakisoma kwenye madarasa yakiwa hayajaezekwa.

Mkurugenzi huyo alisema fedha hizo zilikuwa zimepangwa zitumike kwa ziara ya madiwani kwenda kutembelea Hifadhi ya Wanyama Koga iliyopo mpakani mwa wilaya hiyo na Mkoa wa Katavi.

Alisema madiwani wanatakiwa kupeleka maendeleo kwa wananchi pasipo kubagua dini, kabila na itikadi ya vyama na kuachana na mambo yasiyo ya msingi. 

Habari Kubwa