Bil. 15/- zamweka pabaya mwekezaji

07Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Bil. 15/- zamweka pabaya mwekezaji

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameridhia uamuzi wa kuvunja mkataba wa ukodishaji ardhi hekta 36,432 uliofanywa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) baada ya mwekezaji Kampuni ya Agro Ranch Company Limited kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba.

Mbali na kuridhia kuvunjwa mkataba huo, Mpina amemtaka mwekezaji huyo  alipe fidia ya hasara aliyoisababishia Serikali katika kipindi chote cha uwekezaji wake ya Sh. bilioni 15 huku akimtaka kuondoa mifugo yake katika ranchi na kumuagiza Kaimu Meneja Mkurugenzi wa Narco kuteua meneja wa kusimamia ranchi hiyo na kuweka ulinzi imara.

Mpina amefikia uamuzi huo juzi baada ya kutembelea ranchi zinazomilikiwa na kampuni hiyo za Kagoma hekta 16,313,  Kikulula 11,718,  na Mabale 8,401 na kubaini kuwapo ukiukwaji mkubwa wa makubaliano aliyoingia na Serikali tangu 2012.

Mpina alitaja miongoni mwa makubaliano aliyoingia na Serikali wakati akikodishwa ardhi hiyo ni kujenga machinjio ya kisasa na kiwanda cha nyama ifikapo 2014, kulipa gawiwo kwa Serikali la wastani wa Sh. bilioni 3 kwa mwaka, lakini hadi leo mwekezaji huyo ameshindwa kutekeleza ahadi hizo kuipotezea Serikali mapato ya Sh. bilioni 15. Badala yake mwekezaji huyo amekuwa akilipa Sh. 2,672 kwa ekari sawa na Sh. milioni 240.5 tu mwaka badala ya Sh. bilioni 3 alizoahidi kwenye mkataba.

Pia Mpina alichukizwa na kitendo cha ranchi hiyo kutunza ng’ombe 4,500 wakati uwezo wake ni  ng’ombe 20,000 hadi 30,000.

Aidha, Waziri Mpina alisema mwekezaji huyo amekuwa akitoa visingizio na kwamba uzembe na udanganyifu huo umeisababishia Serikali hasara ya Sh.bilioni 15 pamoja na faida nyingine za kiuchumi na kijamii zitokanazo na uwekezaji huo.

“Kwa kuwa Serikali imepata hasara kubwa na mwekezaji hana tena uwezo wa kuendesha ranchi hizo, tayari nimepitia maamuzi ya Narco ya kuvunja mkataba huo pamoja na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo  nimeridhia mkataba huo kuvunjwa rasmi leo na mwekezaji alipe fidia ya hasara aliyoisababishia Serikali katika kipindi chote cha uwekezaji wake,” alisema.

Alimuagiza Kaimu Meneja Mkuu wa Narco na Mkuu wa Wilaya ya Muleba kumaliza migogoro iliyopo kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka ranchi hizo ambapo alitoa siku 14 kazi hiyo iwe imekamilika na taarifa kuwasilishwa wizarani.

Kaimu Meneja Mkuu wa Narco, Prof. Philemon Wambura, alisema kwa kuwa mwekezaji huyo alishindwa kutekeleza makubaliano, waliamua kuvunja mkataba wake Novemba mwaka huu baada ya kujiridhisha hana uwezo wa kuendeleza ranchi hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Ruyango, alisema ranchi hizo zinakabiliwa na migogoro, ikiwamo ya wananchi kuvamia maeneo. 

Habari Kubwa