Ahimiza ushirikiano kukabili majanga

23May 2019
Salome Kitomari
DAR
Nipashe
Ahimiza ushirikiano kukabili majanga

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dorothy Mwaluko, amesema kuna umuhimu wa ushirikiano wa kikanda na kimataifa kupata misaada ya kiufundi na kifedha katika kukabili majanga ya asili na yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dorothy Mwaluko.

Kwa mujibu wa taarifa yake aliyoiwasilisha kwenye mkutano wa wadau ulioitishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Kupunguza Majanga (UNISDR) hivi karibuni, alisema Tanzania itaendelea kupambana na maafa mbalimbali kwa kuhakikisha usalama wa watu wake.

Majanga hayo ni ukame kupindukia, njaa, mafuriko, vimbunga, matetemeko ya ardhi na mengineyo ambayo huwa na matokeo hasi kwa maisha ya watu, mali, miundombinu na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Alisema kwa miaka miwili iliyopita, serikali imepiga hatua mbalimbali za kutekeleza mkataba wa Sendai wa kupunguza majanga wa mwaka 2015-2030 katika sekta mbalimbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

"Mwaka 2017 serikali ilitengeneza kanuni za kusimamia majanga ikiwa ni mkakati wa kuimarisha uratibu wa majanga na kukabiliana nayo," alisema.

Mwaliko alisema serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuweka kipaumbele, bajeti kwa kadri inavyopatikana, kupunguza majanga na ustahimilivu ikiwa ni pamoja na kuimarisha uchumi.

Alizitaja jitihada mbalimbali zilizofanyika kuwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya usafiri ikiwamo kuongeza usafiri wa majini, ardhi na anga.

Alizitaja jitihada zingine zilizofanyika ni upatikanaji wa huduma za maji safi na salama hususan maeneo ya vijijini, lengo likiwa ni kupunguza majanga kwa watu wa kipato cha chini.

Alisema kwenye upande wa sekta ya afya, serikali imeweka kipaumbele maeneo ya vijijini ambako kuna idadi kubwa ya wakazi, ikiwamo kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kuhakikisha wakati wa majanga wananchi wanapata huduma zote muhimu.

Katibu Mkuu huyo alisema hatua zingine zilizochukuliwa ni kuzuia uchomaji wa misitu ovyo kwa kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya wadau kulinda misitu na mashamba.