Yanga yatakata ugenini Mbeya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:21 AM Sep 26 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Kiungo wa Yanga, Clatous Chama (kulia), akijiandaa kumtoka mchezaji wa KenGold FC, Mashimo Daudi katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya jana. Yanga ilishinda bao 1-0.

BAO pekee lililofungwa na mlinzi wa kati, Ibrahim Hamad 'Bacca', limewapa pointi tatu muhimu mabingwa watetezi, Yanga katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wenyeji KenGold FC iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Sokoine jijini Mbeya jana.

Mchezaji huyo alipachika bao kwa kichwa dakika ya 12, akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa na Stephane Aziz Ki.

Lilikuwa ni bao la kwanza kufungwa kwa kichwa na timu ya Yanga msimu huu, huku likiwa la 57 katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Bacca alifunga bao hilo dakika mbili baada ya kuiokoa Yanga isifungwe goli kutokana na mpira wa kona ulioonekana kuingia moja kwa moja wavuni kufuatia mpira wa kona uliopigwa na Makenzi Ramadhani dakika ya 10, ulionekana unataka kuingia wavuni, lakini beki huyo akipiga kichwa cha nyuma na kuurudisha uwanjani, kuinusuru timu yake.

Katika mechi ya jana ambayo mashabiki wengi walidhani Yanga ingepata mabao mengi, haikuwa hivyo kutokana na KenGold kuonekana kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, wakikaa nyuma ya mpira kwa dakika 70 na kuanza kushambulia dakika 20 za mwisho, lakini bahati haikuwa yao.

Yanga ndiyo ilianza mpira huo na moja kwa moja nusura ipate bao bila wapinzani wao kugusa, baada ya shuti la Clatous Chama kudakwa na kipa wa KenGold, Castor Mhagama, ambaye jana alikuwa shujaa kwa kuokoa michomo ya hatari kutoka kwa mabingwa hao watetezi.

KenGold ikajibu shambulizi hilo dakika ya kwanza, ambapo ilifika katika lango la Yanga, lakini straika wake Ramadhani Chobwedo alishindwa kuuweka mpira wavuni uliokuwa umetua ndani ya eneo la hatari, badala yake alipiga hewa, kabla ya mabeki kuokoa.

Dakika ya pili, Yanga ilihamia tena langoni kwa Yanga na kufanya mashambulizi mawili ya hatari kutoka kwa Chama na Aziz Ki, lakini umahiri wa kipa, Mhagama uliinyima bao.

Clement Mzize alipata nafasi nzuri na kuukwamisha mpira wavuni dakika tano kabla ya kwenda mapumziko baada ya mabeki wa KenGold kujichanganya walipokuwa wakipasiana, lakini akiwa ana kwa ana na Mhagama, alipiga shuti kali lililopanguliwa na kipa huyo na kuwa kosa.

Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko, ambayo kwa kiasi kikubwa yaliisaidia zaidi KenGold na kuanza kuwazoea Yanga, wakiamua kwenda mbele kushambulia.

Kipindi cha pili Yanga iliwatoa Mzize, Chama, Maxi Nzengeli, Aziz Ki na nafasi zao kuchukuliwa na Prince Dube, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahaya na Kenneth Musonda.

Dakika ya 80, Joshua Ibrahim nusura aipatie KenGold bao baada ya shuti lake kupaa juu, na nafasi nzuri zaidi ilipatikana dakika tano kabla ya mechi kumalizika pale Helbert Lukindo alipounganisha mpira wa krosi ya Joshua, lakini mpira ukagonga nguzo ya chini na kuonekana kama unatinga wavuni, lakini ulirejea uwanjani huku benchi la ufundi la timu hiyo likiwa limeanza kushangilia.

Huu ni ushindi wa pili kwa Yanga, michezo yote ikicheza ugenini, ilianza msimu mpya kwa kuwafunga Kagera Sugar mabao 2-0, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera huku KenGold ikipoteza mchezo wa tano mfululizo.

Yanga sasa imepanda hadi nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi sita huku KenGold ikibaki chini kwenye mkia.

Wakati huo huo katika mechi iliyochezwa mapema jana mchana, JKT Tanzania imefikisha pointi sita baada ya kuwafunga Coastal Union mabao 2-1.