SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa ratiba kamili ya raundi ya tatu ya kombe la FA huku klabu za Simba na Yanga zikiwa hazijapangiwa tarehe za michezo yao kutokana na kuwa kwenye michezo ya kimataifa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam, michezo ya raundi ya tatu inatarajiwa kupigwa kuanzia Desemba 5 mpaka 8 mwaka huu, lakini vigogo hao wakiwa wameondolewa kwenye ratiba kwani zote zitakuwa ugenini Algeria kucheza mechi za kimataifa.
Desemba 7, mwaka huu, Yanga itakuwa nchini Algeria kucheza dhidi ya MC Alger kwenye Uwanja wa Julliet wa Tano, saa 4:00 usiku kwenye mchezo wa Kundi A, Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Simba itacheza siku moja baadae (Desemba 8) saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui dhidi ya CS Constantine ya Algeria katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwenye mchezo wa raundi ya tatu ya FA, Yanga ilipaswa icheze dhidi ya Copco FC, huku Simba ikipangiwa dhidi ya Kilimanjaro Wonders Sports Center.
Kwa mujibu wa TFF, tarehe za michezo hiyo itapangwa baadaye huku timu zilizobaki zikitarajiwa kucheza kuanzia Desemba 5 hadi 8.
Azam FC inatarajia kukipiga dhidi ya Iringa Sports, Desemba 7 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Singida Big Stars itakuwa Uwanja wa Liti, Singida kucheza dhidi ya Magnet FC, Mashujaa FC itawakaribisha mabingwa wa Tanzania Bara mwaka 1986, Tukuyu Stars kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, KMC itacheza na Black Six, Uwanja wao wa nyumbani, Fountain Gate itacheza dhidi ya Mweta Sports, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, Coastal Union itakuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuisubiri Stand United, Kagera Sugar na Rhino Rangers zitakipiga kwenye uwanja wa Kaitaba huku Dodoma Jiji ikikipiga na Leo Tena, Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Michezo ya raundi ya tatu itaendelea tena Desemba 8 ambapo Geita Gold itacheza na Ruvu Shooting, Uwanja wa Nyankumbu, Geita, Prisons itacheza dhidi ya Tandika United Uwanja wa Sokoine, Mbeya wakati JKT Tanzania itaumana na Igunga United kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED