Makata afurahia ushindi wa kwanza TZ Prisons

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:33 AM Oct 03 2024

Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata.

KOCHA Mkuu wa Tanzania Prisons, Mbwana Makata, ameeleza kufurahishwa na ushindi wa kwanza kwa timu yake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza michezo sita sawa na dakika 540, akisema huo ni mwanzo tu wa mazuri ambayo yanakuja kwenye timu yake.

Awali Prisons ilicheza dakika 450 bila kupata ushindi, ikiwa ni michezo mitano, ikitoa sare nne na kupoteza mmoja, kabla ya juzi kupata ushindi wa kwanza wa mabao 3-2, dhidi ya Fountain Gate, ikicheza uwanja wake wa nyumbani, Sokoine jijini Mbeya.

Makata, alisema haikuwa rahisi, kwani walikuwa wakitanguliwa kufungwa, lakini mara zote mbili walifanikiwa kusawazisha na hatimaye kupata bao la ushindi.

"Niwapongeze wachezaji wangu, wamepambana kwa kila njia, walicheza wakiwa na uchovu mkubwa kwani tulitoka safarini Ruangwa kucheza na Namungo, katika mchezo huu haikuwa rahisi kushinda kwa sababu tulitanguliwa mara mbili.

Nasema hivi kwa sababu Fountain ni timu ngumu, ina washambuliaji wazuri ambao ukifanya kosa moja wanaweza kukuadhibu," alisema kocha huyo.

Hata hivyo alisema amegundua udhaifu sehemu ya ulinzi kiasi cha kuruhusu mabao mawili ambayo kwa upande wake alisema yalikuwa rahisi sana, hivyo anakwenda kulifanyia kazi.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya, aliwapongeza wapinzani wake kwa ushindi na kuwapa pole viongozi, wachezaji na mashabiki wa timu yake.

"Niipongeze timu iliyoshinda, walikuwa kwenye kiwango bora, nawapa pole viongozi, wachezaji wangu na mashabiki waliotoka Manyara kuja Mbeya kushangilia timu yao," alisema kocha hiyo.

Mabao ya Prisons kwenye mchezo huo yalifungwa na Nurdin Choma kwa mkwaju wa penalti, Ezekia Mwashilindi na Vedastus Mwihambi, huku ya Fountain Gate yakifungwa na Selemani Mwalimu na Kassim Selemani.

Matokeo hayo yanaifanya Prisons kufikisha pointi saba katika michezo sita iliyocheza ikiwa kwenye nafasi ya tisa, Fountain Gate inasalia na pointi zake 13, ikiwa kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo.