Lugano achaguliwa tena Lindi

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:18 AM Sep 27 2024
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Picha: Mtandao
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

HOSEA Lugano amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Lindi (LIREFA), katika uchaguzi uliofanyika mkoani humo juzi.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilichukuliwa na Ahmedi Bongi wakati Rehule Nyaulawa alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya LIREFA walioshinda ni pamoja na Abdallah Kipingo, Ally Ally, Chande Kachele, Sharifa Mkwango na Juma Nandonde, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Rais wa TFF, Wallace Karia, aliipongeza kamati hiyo ya utendaji iliyochaguliwa na kuwataka kusimamia maendeleo ya mpira wa miguu mkoani humo.

Karia ameutaka uongozi huo pia kutekeleza majukumu yao ambayo ni ustawi wa mpira wa miguu ndani ya mkoa huo.

Wakati huo huo, Blassy Kiondo, ametetea nafasi yake ya uenyekiti katika Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Rukwa (RUREFA).

Kanyinki Nsokolo alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti huku Ayubu Nyaulingo akishinda cheo cha Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Richard Ntinda, Goodhope Mushi na Sharifa Mangosongo.