Fountain Gate yatamba kuisulubu Kagera Sugar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:00 AM Sep 27 2024
Kocha wa magolikipa wa timu hiyo, Ally Mustapha 'Barthez',
Picha:Mtandao
Kocha wa magolikipa wa timu hiyo, Ally Mustapha 'Barthez',

LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kuendelea leo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa ulioko Babati, mkoani Manyara kwa Fountain Gate kuikaribisha Kagera Sugar, huku wenyeji wakitamba wamewaandalia wageni kipigo.

Fountain Gate ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikikusanya pointi 10, itaingia uwanjani kucheza dhidi ya Kagera Sugar iliyopata ushindi wa kwanza Ijumaa iliyopita kwa kuwafunga KenGold mabao 2-0, baada ya michezo yake minne ya mwanzo kutoka patupu.

Kocha wa magolikipa wa timu hiyo, Ally Mustapha 'Barthez', amesema wanatarajia kuendeleza walipoishia na kwa sababu wanacheza nyumbani.

Barthez alisema hawataki kuwahuzunisha mashabiki wao ambao wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuwashangilia wanapocheza nyumbani.

"Tumejiandaa vizuri kabisa na mchezo huu, wachezaji wana morali baada ya kupata matokeo mazuri tukiwa ugenini dhidi ya Tabora United, hii imetupa nguvu kubwa sana chini ya mwalimu wetu mkuu, Mohamed Muya, kama kawaida yetu hatutaki kuwahuzumisha mashabiki wetu, huwa wanajitokeza uwanjani na kutushangilia sana na kuwapa wachezaji wetu nguvu kubwa," alisema Barthez.

Naye mchezaji tegemeo, Salum Kihimbwa, alisema siku zote timu hiyo huwa haina maneno mengi, badala yake wachezaji wanaiacha miguu iongee uwanjani.

"Siku zote Fountain Gate hatuna maneno mengi, hatuzungumzwi sana, lakini tunaacha miguu iongeee uwanjani, ila tunawaahidi mashabiki wetu tutaendelea kuwapa furaha, waje kwa wingi uwanjani" alisema Kihimbwa.

Timu hiyo imecheza michezo mitano, ikishinda mitatu, sare moja na imepoteza mechi moja tu ambayo ilikuwa ni ya kwanza kwao dhidi ya Simba, iliyochezwa Agosti 25 na kufungwa mabao 4-0, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Paul Nkata, amesema baada ya kushinda mchezo wao wa kwanza, wachezaji wake wameanza kujiamini, ambapo licha ya kucheza ugenini dhidi ya Fountain Gate, lakini wana uhakika na ushindi.