JIJI la Dar es Salaam sasa linavutia katika baadhi ya masoko ambayo yamemalizika ujenzi na kuleta sura mpya.
Masoko mengi yanayojengwa hivi sasa ni ya ghorofa ambayo hayachukui eneo kubwa la kiwanja na pia kutoa nafasi ya kupata vyumba vingi vya kufanyia biashara hizo.
Kabla majengo hayo ya kisasa hayajajengwa kulikuwa na masoko yaliyojengwa kienyeji ambayo hata miundombinu yake haikuwa rafiki kwa wateja.
Masoko mengi hasa wakati wa mvua yanageuka kuwa kero kutokana na njia za kuingia kwenye masoko hayo kujaa matope na maji machafu.
Pia wafanyabiashara wengi walikuwa hawana maeneo maalumu ya kuuza bidhaa zao hasa wale wadogo na kuishia kuzipanga chini.
Lakini kwa utaratibu huu wa kujenga masoko ya kisasa umesaidia kuwa na nafasi nyingi zinazoweza kuwachukua wafanyabiashara wengi.
Hata hivyo, baada ya masoko hayo kukamilika kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa kwenye masoko hayo toka mwanzo kutopewa kipaumbele kama walivyoahidiwa wakati ujenzi wa majengo mapya ulivyoanza.
Malalamiko yanatokana na wafanyabiashara hao kudai kuwa kuna baadhi ya watu hawakuwapo kwenye soko hilo, lakini sasa wanaonekana na ndio wanaopewa kipaumbele.
Uzoefu wa malalamiko umeanza tangu soko jipya ya Machinga Complex, Ilala Mchikichini, ambapo wafanyabiashara wadogo walilalamika baadhi yao kukosa vizimba, au kupangiwa vya juu ambako wateja wengi hawafiki.
Kituo cha biashara cha Mwenge pia kumekuwa na malalamiko kuwa wafanyabiashara waliokuwapo tangu mwanzo katika eneo hilo ambao waliahidiwa kupewa kipaumbele cha kupewa nafasi, waligeukwa na badala yake wenye uwezo kifedha kupewa kipaumbele.
Hali kama hiyo ilijitokeza katika soko jipya la Kariakoo, ambalo liliungua moto na kujengwa upya, huku wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao hapo, kuahidiwa kuwa wao ndio watakaopewa kipaumbele soko litakapokamilika.
Hata hivyo, malalamiko yale yale yaliyojitokeza katika masoko mengine ndio yanayojitokeza katika soko hilo na kusababisha sintofahamu.
Tatizo kama hilo limejitokeza tena katika soko la Tandale, ambako kumezuka vurugu baada ya wafanyabiashara kulalamika kubadilishiwa maeneo ya kufanyia biashara na viongozi wa soko na Halmashauri ya Manispaa Kinondoni.
Wafanyabiashara hao wameshutumu viongozi wao kwa madai ya kuingiza watu wapya wasio wafahamu.
Sintofahamu hizi zinaweza kusababisha vurugu ambazo zingeweza kuzuilika kama ungewekwa utaratibu mzuri na unaofuatwa.
Kama wafanyabiashara hao waliahidiwa kupewa kipaumbele cha kupata maeneo, iweje baada ya soko kukamilika, utaratibu ukiukwe?
Madai ya wafanyabiashara hao ni kuonekana hawana thamani kuwapo kwenye soko hilo baada ya soko kuwa la kisasa na wanaostahili kufanya biashara ni wenye mwonekano unaofanana na soko hilo.
Ni vizuri viongozi wa soko na manispaa wakakaa pamoja na wafanyabiashara hao kuwaelewesha utaratibu badala ya kupewa lawama ambazo si za kweli.
Kila jambo linahitaji elimu ili watu waelewe kuepusha migongano na sintofahamu ambazo mwishowe husababisha vurugu.
Wafanyabiashara wasikilizwe maoni yao na viongozi watoe majibu ili kupata mwafaka na biashara iendelee kwa faida ya taifa na wananchi wenyewe kuimarisha uchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED