KWA walio wengi kilimo cha mboga ni lazima kuwa na eneo kubwa na lenye nafasi kwa ajili ya kuandaa bustani.
Wakifikiria kuwa kuna kutumia gharama kuliandaa, kununua mbolea, kuandaa vitalu na hata namna bora ya kuweka miundombinu ya umwagiliaji ikiwamo mifereji na mitaro ya kusambaza maji.
Lakini, sasa unaweza kulima mboga nyumbani kwako, kwa kutumia eneo dogo ulilonalo au kuzipanda kwenye makopo kama unavyopanda maua na makasha mbalimbali.
Kwanza kupunguza gharama ya ununuzi wa mboga za nyumbani, pia zinakuwa salama katika kuandaliwa kwani zinalimwa kwa kuzingatia mbinu sahihi za kupanda na kutunzwa hasa kuepuka kemikali.
Baadhi ya wakulima wanakumbana na changamoto ya namna gani anaweza kuandaa mashamba yao ili wapate mimea yenye virutubisho vya kutosha na kufanya mlaji apate kilicho sahihi.
Hiyo ni kutokana na kukosa elimu sahihi ya kuandaa mashamba na bustani kwa ajili ya kupanda mimea, ndio maana mazao hushindwa kustawi vizuri na wakati mwingine kufa.
Jamii imeshuhudia mazao mengi yakishambuliwa na wadudu, kama vile migomba na mboga hali hiyo inapelekea mkulima au mwenye bustani kurudi nyuma kutokana na mimea kuathiriwa.
Kwa upande wa migomba inabadilika rangi na kuwa ya njano na kuuzuia kuzaa matunda na wakati mwingine mgomba kufa.
Hivyo ili mkulima aepukana na adha za mimea kufa, ni vema kufuata hatua sahihi za kupanda mimea au kundaa mashamba, bustani kwa ajili ya kupanda mazao yenye virutubisho.
Kwa mujibu wa mtalamu wa kilimo, Salimu Hussen, anyeuza pembejeo za kilimo Mwenge jijini Dar es Salaam, baadhi ya wakulima hulima na kupanda mazao, pasipokujua kwenye ardhi hiyo kuna minyoo au virusi vinavyoweza kushambulia mazao yao.
Aidha, anasema mkulima anapoandaa shamba au bustani ni vema akapata elimu sahihi, katika kuandaa kwa kutumia dawa za kurutubisha ardhi na kuua virusi na vimelea waliopo kabla ya kupanda mimea.
Anaendelea kwa kusema ardhi zimetofautiana, kuna ardhi zenye unyevu na zingine hazina hivyo dawa hizo husaidia kuiweka sawa na kuwa na virutubisho tayari kupokea mimea yenye kutoa mazao.
Anakumbusha kuwa mbolea ya samadi inarutubisha udongo, mfano sehemu yenye kichanga inaweza kuirekebisha na kuwa bora yenye rutuba kwa ajili ya mazao mbalimbali.
Ukiachilia mbali mbolea ya samadi ya wanyama, mbolea zilizothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ni muhimu kwa kukuzia mazao kwani zina virutubisho vinavyostahili.
Kwa kutambua hili serikali imeshusha bei ya pembejeo za kilimo kwa kutoa ruzuku, kwa kila mkulima atakayejiunga na kuwa na namba ya usajili atanunua kwa bei ya punguzo ndiyo ruzuku.
Sote tunatambua ili kilimo kiwe bora ni lazima kutumia mbolea na dawa za kuwa wadudu kabla ya kupanda mbegu, hivyo serikali imewarahishia wakulima kwa kuweka punguzo kwenye pembejeo za kilimo.
Mtaalamu wa kilimo Hussen, anasema mfuko wa kilo 50 unatumika kwenye heka moja ya shamba na kujitosheleza kustawisha mimea.
Oktoba 2022, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, anawataka maofisa ugani kuhimiza kufanya operesheni ya kujiwekea malengo, kwamba kwa siku lazima wasajiliwe wakulima 50 katika mfuko wa pembejeo za kilimo.
Ingawa anasema kuwa ana imani inawezekana kusajili wengi zaidi ya hao, hiyo ni kutokana na Watanzania walio wengi ni wakulima na wanatumia gharama kubwa kununua pembejeo za kilimo.
Anayasema hayo kwenye kikao kilichohusisha, wakuu wa wilaya, wakurugezi wa halmashauri zote za jiji pamoja na maofisa ugani wa mkoa huo.
Hivyo kuweka utaratibu wa kuweka bei rafiki ya kununua mbolea yenye ruzuku kwa wakulima, ili kupanua wigo wa kilimo na kuwawekea mazingira ya kuwavutia watanzania kujiwekeza kwenye kilimo.
Mratibu wa Mradi wa FRESH unaoshughulika na kilimo cha mboga wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Mikocheni, Dar es Salaam, Dk. Violeth Mwaijande, anazungumzia matumizi ya mbolea.
|Anasema endapo mkulima ataweka mbolea ya chumvichumvi kwenye mboga na kukaa zaidi ya siku tatu kabla ya kuichuma hakuna madhara yatokanayo na mbolea hiyo,
Mtaalamu huyo anasema kuwa ni vema mkulima akatumia mbolea ya samadi mara ya kwanza, halafu atumie ya chumvichumvi, ili kusaidia mmea kustawi vizuri na kuchocheo kutoa majani mengi.
Pia anaeleza ni vizuri mbolea ya samadi iwe imeoza na sikutumia mbichi ambayo huunguza mimea kwasababu ina moto hivyo haifai kutumiwa, hasa kwenye kilimo cha mboga.
KUANDAA KITALU
Utayarishaji wa kitalu cha mboga unajumuisha mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandaa shamba mfano usafi kwa kuondoa magugu na vichaka vinavyozunguka.
Kadhalika kuweka dawa ya kuondoa magugu, kwasababu magugu huua mimea, husababisha isiote wala kustawi vizuri kwani inaizingira na endapo mkulima atatumia njia za kisasa anatajipatia mavuno mengi.
Mtaalamu wa kilimo wa TARI, Dk. Violeth anawataka kuhakikisha upatikanaji wa maji, kuweka mifereji, njia za kuleta maji au kuhifadhi maji kwa kutengeneza kisima au matangi.
Anasema ni vizuri kutenga eneo maalumu kwa ajili ya kuhifadhi na kuchanganya mbolea shambani au bustanini.
Vile vile Dk. Violeth anashauri kutifua kwa jembe eneo unalootesha miche, au kusia mbegu pia bila kusahau kuangamiza wadudu na magonjwa yatokanayo na udongo.
Anasema kabla ya kutayarisha matuta ya kitalu ni lazima kutumia dawa ya kunyunyiza katika udongo, kuharibu wadudu waharibifu.
“ Unaweza kuchoma udongo au kufunika eneo la tuta la kitalu kwa kutumia plastiki inayopitisha mwanga kwa wiki mbili hadi nne ili kuua wadudu na minyoo udongoni ambayo itapelekea mimea isistawi kikamilifu.” Anasema Dk. Violeth.
Anatoa wito kwa wakulima kutumia bustani za maua kwa kupanda mboga na kuachana na dhana kuwa maua yanapendezesha nyumba, kwani mboga pia ni kivutio.
Vile vile inapaswa wafahamu kuwa hata mboga zikipandwa kwa ustadi zinapendezesha nyumba, kuondokana na gharama za kununua mboga masokoni ambazo haifahamiki zilivyoandaliwa.
Dk. Violeth pia anawashauri kutumia mbolea ya chumvichumvi kwani serikali imeweka punguzo la bei ili mkulima amudu mbolea hiyo na kuondokana na dhana ya kuwa mbolea hiyo ina madhara wakati ina virutubisho kwenye mmea.
IMEANDIKWA NA TUNTULE SWEBE, JOYCE LAMECK
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED