NCHINI hadi sasa, kuna hofu imetawala kuwapo matukio ya kikatili yakiripotiwa kwenye vyombo rasmi na mazungumzo tofauti, yakihusisha mauaji ya watoto kwenye maeneo tofauti.
Hiyo ni katika kipindi takriban miezi sita, hata kusababisha hofu kwa baadhi ya wazazi na walezi na makundi mengineyo ya malezi ya kijamii. Ushuhuda wake uko pia kwenye mijadala ya mitandao ya kijamii, wazazi na walezi hawana amani.
Ni hali inayojumuisha umma kutawaliwa na hofu inayojengwa na ukweli, familia za watu wa kipato cha kati na chini kumudu ulinzi wa usalama wa watoto saa 24, hasa kwa kuwa ukatili hauna eneo maalum unapotendwa unaweza kuwa shule, njiani au nyumbani.
Miongoni mwa matukio ya kikatili yanatotajwa kutokea ni pamoja na lile linalohusisha dada msaidizi wa kazi za nyumbani, anayedaiwa kumkata shingo mtoto wa mwajiri wake.
Tukio hilo lilitokea Julai 17, 2024, dada huyo kumjeruhi shingoni kwa kitu chenye ncha kali mtoto anayeishi eneo la Goba Kinzudi, Kinondoni kisha mtuhumiwa akadaiwa kukimbia, lakini tayari Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limefanikiwa kumkamata.
Tukio hilo linafuatia mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe, aliyekuwa na umri miaka miwili na nusu yaliyotokea mkoani Kagera. Inadaiwa mtoto huyo alitekwa na watu wasiofahamika Mei 30, 2024 nyumbani kwao kijiji cha Mulamula wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Mwili wa mtoto huyo ulipatikana Juni 17, 2024 ukiwa umenyofolewa baadhi ya viungo. Miongoni mwa watu tisa wanaoshtakiwa kuhusu mauaji ya mtoto huyo, yupo baba mzazi.
Washtakiwa wengine yumo Padre miongoni mwa waliofikishwa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba,.
Pia, kuna matukio mengine kadhaa yanayohusisha watoto kutoweka na kukutwa wakiwa wamekufa na kunyofolewa viungo kwenye miili yao.
Ndio katika mazingira kama hayo, hofu inatawala zaidi hasa watu ambao wanatarajiwa kuwa viongozi, wa kuzuia na wakemeaji wa ukatili wanapotajwa kuhusishwa na matukio ya aina hii, Ni hali inayoibua makundi ya kijamii, bila kujali dini, kabila wala vyama vya siasa, kuunganisha nguvu za pamoja katika kusaka suluhisho la kukomesha vitendo hivyo vya kikatili, vimekuwa vikiibuka zaidi hasa wakati ambapo uchaguzi za viongozi wa kisiasa zinapokaribia.
Hilo linajenga mazingira ya viongozi wa kisiasa na serikali za mitaa kujitokeza kuonyesha uwezo wao wa uongozi kwa kuwaunganisha wananchi katika maeneo yao kujadili njia bora ya kuzuia ma kukomesha matukio ya kikatili.
Ni hali watoto wanakosa utulivu na amani kwa habari za matukio hayo, hivyo wanaweza kushindwa kufanya vizuri hata kwenye masomo yao.
Pia kwa baadhi ya wazazi na walezi wa kipato cha kati na cha chini watoto wanakwenda na kurejea kutoka shule wakijitegemea iwe kwa usafiri wa umma au kwa miguu kulingana na umbali wa shule anayosoma mtoto husika nao wanakosa utulivu wa kushiriki vyema kujitafutia kipato.
SHERIA ZINAKOSIMAMA
Sheria ya Mtoto Mwaka 2009, ni waraka unaoshughulikia masuala mengi kitaifa yanayohusu haki na ulinzi wa mtoto. Hiyo, pia inachukua mikataba na makubaliano yanayohusu haki za mtoto kwa ujumla.
Inalenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za watoto nchini hapa, imeainisha haki ya mtoto kulelewa na wazazi, haki ya kupewa jina kuwa na utaifa, haki ya kupata mahitaji ya msingi kama chakula, malazi, mavazi, matibabu, chanjo, elimu, na haki ya kucheza na kuburudika.
Asasi ya World Vision Tanzania, inabainisha kuwa jukumu la ulinzi wa mtoto ulinzi na usalama wa mtoto sio jukumu la maafisa wa ustawi wa jamii peke yao ni jukumu la Taifa kwa ujumla. Hakuna anayeruhusiwa kumdhuru, kumumiza au kumnyonya mtoto.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF), nalo katika katika utafiti uliotolewa Januari 15, 2024 linabainisha kuwa duniani kote mwaka 2024, watoto wanatarajiwa kuona kuongezeka kwa matukio ya ghasia, vita na matatizo ya kiuchumi.
Kila mwanzo wa mwaka, UNICEF huchunguza hatari ambazo watoto wanaweza kukumbana/ kukabiliana nazo, na kupendekeza njia za kupunguza madhara yanayoweza kutokea.
Katika ripoti hiyo inayoitwa Matarajio ya Watoto 2024: Ushirikiano katika Ulimwengu uliogawanyika, pamoja na mambo mengine kadhaa inabainisha katika uchaguzi wa mwaka 2024, na demokrasia ya kimataifa itakabiliwa na hatari ambazo hazijawahi kushuhudiwa, zinazotolewa na taarifa potofu na vurugu za kisiasa, zinazotishia haki na huduma za watoto.
Inaelezwa kuwa watoto na vijana wanaweza kuathiriwa zaidi na unyanyasaji huu, ambao unaweza kusababisha kifo, madhara ya kimwili au ya kihisia, kukatizwa kwa huduma za umma na kufungwa kwa shule, vijana wanaonyesha kutoridhika na demokrasia, lakini wanaelekeza nguvu zao katika hatua za kujenga za kiraia, na uharakati wa mtandaoni.
Pia, kuna athari za ukuaji usiokubalika wa teknolojia ikiwa ni pamoja na zinachochea hofu na wasiwasi kuhusu ustawi wa watoto, sera ya udhibiti unaokuja ikiwa itazingatia mahitaji ya watoto na kubuniwa kwa uwajibikaji, unaweza kutoa fursa na kupunguza athari hasi.
Inaelekeza njia ya kuwalinda watoto, inasema ripoti hiyo, ni mshikamano wa kiuchumi, ushirikiano wa soko, na uwekezaji katika stadi za siku zijazo.
Kuna Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi Ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa: 2017/18 – 2021/22) ni vyema kuwe na mrejesho mzuri wa utekelezaji wa mpango huu.
Imebainishwa kuwa kwa vipindi tofauti kuanzia mwaka 2000 Serikali kwa kushirikiana na wadau ilikuwa ikitekeleza mipango nane iliyolenga kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto, ikiwa ni jitihada za kuleta usawa katika jamii, ambayo pamoja na mafanikio yaliyopatikana kuzuiaa ukatili kwa wanawake na watoto na utoaji huduma kwa waathirika wa vitendo hivyo.
Utekelezaji wa mipango hiyo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo upungufu katika uratibu na upatikanaji wa taarifa za uhakika za vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto nchini.
Kwa mujibu wa MTAKUWWA, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Kamati Elekezi ya Ulinzi wa Wanawake na Watoto Ngazi ya Taifa.
Ni kamati hii inalo jukumu la kutoa miongozo ya kisera na kuratibu utekelezaji wake, pamoja na shughuli za utoaji huduma kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.
Katibu wa kamati hioyo ni Katibu Mkuu wa Wizara yenye dhamana ya kusimamia masuala ya Wanawake na Watoto.
Katika hali hiyo, elimu inahitajika, pia na hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa kwa wazazi wazembe ili watambue wajibu wao wa ulinzi kwa watoto wao, wapo wanaoendekeza anasa na kusababisha watoto kukosa haki ya kulindwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED