Matumaini, kicheko umeme kuifanya Kigoma kitovu cha uchumi na biashara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:08 AM Sep 27 2024
1.	Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (kushoto) akiweka jiwe la msingi katika mradi wa Kufua Umeme Mto Malagarasi MW 49.5 mkoani Kigoma. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Thobias Andengenye.
PICHA; MAKTABA
1. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (kushoto) akiweka jiwe la msingi katika mradi wa Kufua Umeme Mto Malagarasi MW 49.5 mkoani Kigoma. Kulia ni Mkuu wa Mkoa huo, Thobias Andengenye.

SEPTEMBA 19, 2024 ilikuwa siku ya kihistoria katika mkoa wa Kigoma. Ilikuwa siku ya kufungua ukurasa mpya kwa sura ya mkoa huo ambao kwa miaka mingi umekuwa nyuma kiuchumi licha ya kuwa na fursa mbalimbali ambazo zingeufanya kuwa juu kimaendeleo.

Miongoni mwa sababu zilizofanya mkoa huo kuwa katika hali hiyo ni miundombinu ya usafiri hasa barabara na kukosekana kwa umeme wa uhakika ambao ungechochea uwapo wa viwanda vya kuchakata bidhaaa mbalimbali na kutoa ajira za moja kwa moja na sizizo za moja kwa moja. 

Katika suala la usafiri Kigoma ilikuwa ikitegemea zaidi reli ya kati ambayo inaishia hapo kutoka Dar es Salaam ndiyo maana ikapewa jina la ‘Mwisho wa Reli’. Hata hivyo, usafiri huo kwa miaka kadhaa haukuwa wa uhakika kutokana na kuyumba kiutendaji kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC). 

Pia usafiri wa ndege umekuwa tegemeo kwa wananchi wa mkoa huo lakini nao umekuwa si wa uhakika na si wananchi wote wana uwezo wa kutumia aina hiyo. Sababu kubwa ni hali ya kiuchumi kwa kuwa wenye uwezo wa kumudu gharama za usafiri huo ni wachache.  

Kuwapo kwa changamoto ya aina hizo za usafiri, kuliwalazimu watu wanaokwenda na kutoka Kigoma kwenda mikoa mbalimbali kutumia barabara ambazo nazo hazikuwa za lami. Waliotumia usafiri huo walipata shida njiani kutokana na ubovu wa barabara, mabasi yaliyokuwa yakienda na kutoka huko yalikuwa mabovu kiasi cha kuwafanya wasafiri kutumia hata  siku tatu njiani. 

"Enzi zile kabla ya barabara za lami, haikuwa shida ukiwa Mwanza au Dar es Salaam kumtambua mtu aliyekuwa akitoka Kigoma. Ulikuwa unamtambua kwa vumbi tu lakini sasa ni historia,” alisema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, wakati wa uwekaji mawe ya msingi ya mradi wa kuzalisha umeme katika mto maporomoko ya Malagarasi na kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme wa gridi ya taifa cha Kidahwe.  

Kutokana na changamoto hizo, serikali ilifanya jitihada za kuifungua Kigoma kwa aina zote za usafiri ili kuchochea kasi ya maendeleo na kuwa kitovu cha maendeleo.  

Mkoa sasa umefunguliwa kwa barabara za lami na sasa kuna usafiri wa uhakika kutoka kona zote kuingia Kigoma. Waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kupitia Kasulu, umbali wa kilometa 1,298 wanatumia wastani wa saa 18. Kwa wale wa kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma kupitia Tabora, wanatumia saa 19 hadi 20 kutokana na baadhi ya maeneo kutokukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami. 

 Jitihada zaidi zinaendelea kuifungua Kigoma kwa reli ya kisasa (SGR) ambayo kwa sasa ujenzi umekamilika kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kazi inaendelea Makutopora (Dodoma) hadi Tabora na hatimaye Kigoma. Usafiri huo utakapoanza utaifungua zaidi Kigoma na kupanua fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

    HATIMAYE UMEME 

"Sasa umeme wa uhakika wa gridi ya taifa unaanza kuingia Kigoma. Ile historia ya kuwa moja ya mikoa iliyo nyuma kiuchumi inafutika. Tulianza na barabara, tunakuja na umeme hatimaye treni ya kisasa (SGR). Nuru inawaka Kigoma," alisema Dk. Biteko.

Kama ilivyokuwa kwa mikoa ya pembezoni kama Kagera, Rukwa na Katavi, Kigoma ilikuwa ikitumia majenerata kuzalisha umeme hali ambayo ililisababishia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) gharama kubwa za uendeshaji na kuliingizia hasara. 

Kwa mujibu wa Dk. Biteko, kwa mwaka TANESCO imekuwa inatumia Sh. bilioni 35 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta mazito ambayo hutumika kwa ajili ya kuzalisha umeme.

 "Pamoja na kutumia fedha hizo, ukiangalia kiasi kinachopatikana kwa ajili ya kuuza umeme ni Sh. Bilioni 16, hivyo shirika linapata hasara ya Sh. bilioni 19. Kwa hiyo ulikuwa mzigo mkubwa na sasa tutauondoa," alisema.

 Licha ya matarajio ya kupata umeme wa gridi ya taifa megawati 49.5 baada ya kukamilika kwa mradi huo, Kigoma pia itaanza kupata umeme wa gridi ya taifa katika njia zingine hali itakayowezesha kuufungua zaidi mkoa kiuchumi. 

 Kwa hatua hiyo, Kigoma iliyokuwa moja ya mikoa ya pembezoni sasa itageuka kuwa kitovu cha nishati na itaufanya mkoa kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 "Kigoma sasa itafunguka kimaendeleo kwa sababu ya umeme wa gridi ya taifa. Baada ya kufunguka kwa miundombinu ya usafiri, sasa ni zamu ya kufunguka kwa umeme na hatua hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kasi ya maendeleo katika nyanja mbalimbali,” alisema. 

 Katika kufanikisha azma ya Kigoma kuwa kitovu cha nishati, serikali imetoa Sh. trilioni 1.2 ambazo pamoja na ujenzi wa mradi wa Malagarasi, zitatumika kupokea, kupoza na kusafirisha umeme kutoka Nyakanazi kilovoti 620, ujenzi wa njia ya Tabora - Uvinza hadi Kigoma, Katavi hadi Uvinza kilovoti 220 kwa ajili ya treni ya SGR. 

 KAULI YA TANESCO 

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Boniface Nyamohanga, alisema 

umeme wa gridi ya taifa utalipunguzia mzigo shirika wa uzalishaji na kuwa na umeme wa hakika ambao utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa mkoa, maisha bora ya wananchi na pato la taifa. 

 "Umeme huu pia utasaidia kuboresha huduma za kijamii kama elimu na afya. Pia utatengeneza ajira za muda mfupi na mrefu. Zaidi ya wafanyakazi 700 wanatarajiwa kuajiriwa.

 "Licha ya manufaa hayo, gharama za uzalishaji wa umeme zitapungua kwani tutaondoa majereta ambayo yalikuwa yakitumika kuzalisha umeme ambayo yalikuwa mzigo mkubwa kwa shirika.

 “Kigoma ni moja ya mikoa ambayo ilikuwa haijaunganishwa na gridi ya taifa, hivyo kupata umeme kupitia mitambo ya uzalishaji inayotumia mafuta ambayo imekuwa ikiligharimu Shirika fedha nyingi kwa ajili ya uendeshaji na hasa mafuta ambayo miezi ya hivi karibuni bei zake duniani zimekuwa zikipanda.  

 “Kwa upande wa Kigoma mjini, umeme unazalishwa kwa kutumia mitambo ya mafuta iliyopo Kigoma (Megawati 8.75) na pia umeme wa jua unaozalishwa (kiwango cha juu Megawati 4.7) kutoka kwa kampuni binafsi NextGen Solar (SOLAWAZI),” alisema.

 Kuhusu Kasulu na Kibondo, alisema  umeme ulikuwa unazalishwa kwa kutumia mitambo ya mafuta iliyoko Kasulu (Megawati 3.75) na Kibondo (Megawati 2.5) huku akibainisha kwamba mitambo ya Kasulu pia ilikuwa inapeleka umeme katika wilaya ya Buhigwe.

 Kwa mujibu wa Mhandisi huyo, gharama za uendeshaji kwa wastani kwa mwaka katika wilaya ya Kibondo zilikuwa Sh.bilioni 9.44, Kasulu (Sh.bilioni 12.94na Kigoma mjini ni Sh. bilioni 35.78, hivyo kufanya jumla ya gharama kuwa Sh. 58.16 kwa mkoa mzima.

 “Mapato ya mauzo ya umeme kwa mkoa wa Kigoma ni wastani wa Sh. bilioni 16.09 ambayo ni chini ya asilimia 30 ya gharama yote inayotumika kuzalishia umeme huo,” alisema nak ubainisha kuwa kwa sasa kuna unafuu wa kupungua kwa mzigo huo wa gharama baada ya mkoa kuanza kupata umeme wa gridi ya taifa.

“Kwa sasa, maeneo ya Kasulu, Kibondo na Buhigwe yanapata umeme wa Gridi ya Taifa kupitia njia ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Nyakanazi, hivyo kuwezesha shirika kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 22.38 kwa mwaka,” alisema Nyamohanga. 

 Kuhusu mradi wa Malagarasi, Nyamohanga alisema ni Dola za Marekani Milioni 144.14 (takribani Sh. bilioni 389) ambazo serikali  inagharamia Dola za Marekani milioni 4.14 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inagharamia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 140.

 Kwa mujibu wa Nyamohanga, kukamilika kwa mradi huo kutawezesha  kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mkoa wa Kigoma na mikoa jirani, hivyo kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kuchochea maendeleo ya mkoa sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji wa shirika kwa kuondoa majenereta.

 KUZIMWA MAJENERETA 

Kutokana na jitihada hizo, Biteko aliagiza shirika kuzima majenereta yanayotumika kuzalisha umeme ifikapo mwishoni mwa mwaka huu huku wakati wa hafla hiyo kukiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali likiwamo lililosomeka: ”Mradi ukikamilika tutazima majenereta na kuwasha umeme wa gridi ya taifa.”

Bango lingine lilisomeka: “Kuunga Kigoma kwenye gridi ya taifa kutaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme.” Hali hiyo inaweka matumaini mapya ya mkoa wa Kigoma kupata umeme wa uhakika ambao utazaa neema tele za kimaendeleo katika sekta mbalimbali.  

KUFUNGUKA KIUCHUMI 

“Umeme wa uhakika kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi.” Hilo ni bango lingine ambalo linaonesha moja ya mafanikio yanayoweza kupatikana kutokana na uwapo wa umeme huku lingine likisema: “Kukamilika kwa mradi kutaifungua Kigoma kiuchumi.”

Ujumbe huo unahanikizwa na kauli ya Mkuu wa Mkoa, Thobias Andengenye, kwamba hatua hiyo itaifungua Kigoma na kuwa kitovu cha Uchumi na biashara huku akisisitiza kuwa mradi huo utaondoa changamoto za kiuchumi zilizosababisha mkoa kurudi nyuma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zaynab Katimba, ambaye pia ni mzaliwa wa Kigoma, alisema katika hafla hiyo kuwa ujio wa umeme wa gridi ya taifa, unaifanya Kigoma kung’ara katika sekta mbalimbali zikiwamo za uchumi na kijamii. 

“Kwa jumla, wanufaika wakubwa wa umeme ni TAMISEMI kwa sababu ndio wasimamizi wa sekta za elimu na afya. Ukienda katika afya, umeme unahitajika kwa sababu kuna mashine za maabara na vipimo ambazo zinahitaji umeme. 

“Pia katika elimu, kuna maabara ambazo vifaa vyake vinahitaji umeme. Kwa kweli ujio huu wa umeme wa gridi ya taifa utainufaisha Kigoma katika sekta hizo. Lakini pia utachochea maendeleo ya viwanda na kuufanya mkoa wa Kigoma kuwa katika chati ya juu kimaendeleo,” alisema Katimba.       

Ni ukweli kwamba Kigoma ni mkoa wa kimkakati katika biashara kutokana na kupakana na nchi jirani za Burundi na Jamhuri yua Kidemkorasi ya Congo (DRC). Kwa hiyo uwapo wa miundombinu bora ya usafiri na umeme wa uhakika, utachochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa mkoa na pato la taifa kwa ujumla.