KILICHOWABEBA RAIS AKAWASIFIA... Mapinduzi maji Tanga kutoka hatari ukame, hadi mwelekeo kujitosheleza

By Cheji Bakari , Nipashe
Published at 07:59 AM Sep 19 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA),Mhandisi Geofrey Hilly (wa tatu kushoto), akitoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk.Batilda Buriani.
PICHA: CHEJI BAKARI
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA),Mhandisi Geofrey Hilly (wa tatu kushoto), akitoa maelezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk.Batilda Buriani.

MIONGONI mwa vivutio vikubwa katika mazingira, ni uwapo wa vyanzo vya maji vya aina mbalimbali na kwa wastani mkubwa, ndio unajenga maisha ya mwanadamu.

Na inapotajwa dhana ya vyanzo vya maji, ni maeneo yote ambayo maji huanza, kabla ya kusafiri kwenda sehemu nyinginezo. 

Mkoani hapa hivi karibuni, Kamati ya Kudumu ya Bunge Maji na Mazingira ilifanya ziara ya siku moja mkoani Tanga ilitembelea Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga UWASA lengo ni kukagua jinsi fedha zilizotolewa na serikali kutekeleza miradi ya maji.

Kamati hiyo, pia ilitembelea na kukagua idara mbalimbali za mamlaka hiyo, ikiwamo Bwawa la Kuhifadhi Maji la Mabayani linalokusanya maji kutoka chanzo kikuu cha Mto Zigi, unaonzia milima ya Usambara - Tao la Mashariki katika Tarafa ya Amani wilayani Muheza.

Pia, ikatembelea Kituo cha Kutibu na Kusafishia Maji cha Mowe, vyote katika Kijiji cha Pande, nje kidogo ya Jiji la Tanga. 

Katika ziara hiyo, kamati ilivutiwa na jinsi mamlaka hiyo ilifanikisha mpango wake wa kuvilinda na kuvitunza vyanzo vyake vya maji ikiwa na faida nyingi jamii kwa jamii inayoishi kandokando ya vyanzo hivyo. 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jackson Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, anasema kamati yake imefurahishwa na mpango huo, ambao mamlaka hiyo inatunza rasilimali maji. 

" Sisi kamati kazi yetu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji, kupitia fedha mbalimbali zilizotolewa na serikali na zile za hatifungani, ili kutimiza falsafa ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani," anatamka Kiswaga.

UWASA INAVYOWAJIBIKA

Katika hatua zake kukabili uhaba wa maji, UWASA ilianzisha afua mbalimbali za kutunza vyanzo vya maji, ikiwamo katika Mto Zigi, baada ya watu kuvamia chanzo cha mto huo katika Milima ya Usambara, lengo lao ni kutafuta madini ya dhahabu.

Shughuli hizo kwa asilimia kubwa, zilisababisha uchafuzi wa mazingira na kupunguza kina cha maji katika mto huo, hali ambayo wadau wa mazingira waliingilia kati kwa kuanzisha afua mbalimbali za kuhifadhi mazingira.

Hiyo ikaendana na kuweka ulinzi shirikishi na kutoa elimu kwa jamii ya vijiji vinavyozunguka mto huo jinsi ya kutunza mazingira. 

Namna ilivyofanikisha, ilianzisha vikundi vya wakulima na Wahifadhi Mazingira Kihuhwi na Zigi (UWAMAKIZI), waliowapa elimu jinsi ya kufanya kilimo rafiki wa mazingira, pasipo kuathiri vyanzo vya maji.

Ilikuwa ni zao la elimu waliopewa, hata wananchi wananchi walijiunga katika vikundi na kulima mazao ambayo ni rafiki wa mazingira, hata yamenufika upande huo kiuchumi. 

Pia, faida nyingine jambo hilo limeongeza kina cha maji, kupunguza tope mtoni pamoja na uchafuzi wa maji ambapo ilifanya mamlaka hiyo kutumia fedha nyingi kununua kemikali za kusafisha maji kabla ya kuwapelekea wateja jambo ambalo iliwalazimu kuongeza fedha za ankara za maji.

Katika utekelezaji wake, ni kwamba kukawekwa mawe ya mipaka inayozunguka bwawa la Mabayani, linalokusanya maji kutoka chanzo kikuu cha Mto Zigi, ili kuzuia shughuli za kibinadamu.

Mafanikio hayo yameifanya serikali kuipa majukumu mamlaka hiyo kutekeleza miradi mbalimbali ya maji kwa mkoa huo, ukiteuliwa kuwa mkoa wa kimkakati, ikibashiriwa idadi ya wakazi itazidi kuongezeka.

WAZIRI WA MAJI

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ambaye pia ni mbunge mkoani hapa, anasema tayari mamlaka hiyo imeshatia saini mikataba na makandarasi wawili kuboresha mtandao wa majisafi na taka katika jiji la Tanga, baada ya kupata takribani shilingi bilioni 54, kupitia Hatifungani ya Kijani.

Anasema mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Oktoba mwaka ujao, ikiongeza lita kati ya milioni 45 hadi milioni 60 ya maji  ukinufaisha watu 600,000.

"Hizi fedha za hatifungani zinatarajiwa kunufaisha wakazi wa maeneo ya miji ya Tanga, Mkinga, Muheza na Pangani..." anasema.

UPATIKANAJI MAJI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, anasema maji yanapatikana kimkoa, kati ya asilimia 59 hadi 60 kwa wilaya zote nane za mkoa huo na dira ya serikali ni kuhakikisha hadi mwakani maji yaopatikane kwa asilimia 95 ya mahitaji mijini na vijijini asilimia 85.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga (UWASA), Mhandisi Geofrey Hilly, anamuunga mkono Mkuu wa Mkoa akisema kukamilika kwa mradi huo wa kimkakati, upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Tanga kufikia upeo wa juu zaidi ya makadirio yaliyoko.

Mhandisi Hilly, anasema imeingia mkataba na kampuni inayosimamia ujenzi wa Bomba la Mafuta (EACOP), katika kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wilaya za Muheza na Tanga.

Mhandisi Hilly, anasema kuwa fedha hizo zitatekeleza miradi miwili ya maji, matokeo yake ni kunufaisha wananchi 30,000 kwa huduma hiyo.

Msimamizi wa Ujenzi wa EACOP Kituo cha Tanga, Jerome Betat, anasema mradi huo ni sehemu ya kurudishia faida jamii jirani na mradi.

Mnamo Machi mwaka 2021, Dk. Samia alipokuwa  Makamu wa Rais, aliweka jiwe la msingi la Mradi wa Kuboresha Huduma ya Majisafi katika Mji wa Muheza wenye thamani ya Sh. bilioni 6.1, kukabili changamoto ya upatikanaji maji uliokuwa katika mji wa Muheza na vijiji jirani. 

Hivi karibuni, Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango, amezindua Uuzaji Hati Fungani ya Kijani ya (Tanga UWASA) yenye thamani Sh. bilioni 53.12, akisifu kitendo chake cha kutafuta uwezeshaji wa kifedha mbadala, unafaa kuigwa na taasisi zote nchini.

Ni kauli inayorejea alichotamka Rais Dk. Samia, kwa kuisifu mamlaka hiyo kwa ubunifu, ikiendesha shughuli zake katika namna ya ubunifu.

Ugeni wa Dk. Mpango katika hatifungani, ulitanguliwa na uwekaji jiwe la msingi la Mradi wa Kuboresha Hali ya Upatikanaji wa Maji jijini Tanga na Wilaya ya Mkinga, wenye thamani Sh. bilioni 53.12 akisema kitendo cha mamlaka hiyo kuamua kutafuta uwezeshaji mbadala ya fedha ni kitendo cha maendeleo.