Afrika Mashariki ndani ya usukani wa Dk.Ruto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:32 AM Dec 11 2024

Rais wa Kenya, William Ruto.
Picha:Mtandao
Rais wa Kenya, William Ruto.

RAIS wa Kenya, William Ruto, hivi karibuni amekabidhiwa kiti cha kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akichukua nafasi hiyo kutoka kwa mwenzake, Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, baada ya muhula wa mwaka mmoja kukamilika.

Ruto ndiye msimamizi wa jumuiya hiyo, yenye wanachama wanane, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda

Kwa nafasi hiyo, Ruto ataiongoza jumuiya kwa kipindi cha mwaka mmoja, wa mujibu wa  kanuni za EAC kuhusu uongozi wa uenyekiti.

Hivi karibuni jijini Arusha, kwenye mkutano wa 24 wa Marais wa Mataifa wanachama wa EAC, Rais Ruto, kwanza alimpongeza mtangulizi wake akisema ni ‘uongozi wenye kuigwa’ kwa kuwa ulisheheni maono.

“Chini ya uongozi wake, jumuiya ya EAC imepiga hatua kubwa katika kuendeleza misingi ya utangamano,” nasifu Rais Ruto.

AJENDA ZA KUSIMAMIA

Rais Ruto anachukua uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kuzingatia ajenda ya wanachama wote wanane kwa kubuni utangamano wa kisiasa.

“Ndoto ya utangamano wa kisiasa katika EAC ni safari ya kipekee ya kuunganisha eneo hili,” Rais Ruto,  anasema huku akitaja kuwa kuna changamoto ambazo lazima zikabiliwe, ili kufikia lengo hilo.

Rais Ruto anasema kuna manufaa makubwa katika umoja wa kisiasa baina ya mataifa hayo, wanachama wa EAC, kuliko changamoto.

“Sharti kujizatiti kufaidi kutokana manufaa yanayoletwa na hatua hii ili kujenga EAC thabiti ambayo itawezesha kubuniwa kwa soko la pamoja barani Afrika,” anaeleza.

Rais Ruto anaahidi kuwa wakati wa hatamu yake kama mwanachama wa EAC, ataipa kipaumbele ajenda ya kuboresha maisha ya watu wa kwenye ukanda huo wenye takribani watu milioni 332.

Takwimu za tovuti kadhaa mtandaoni zinabainisha kuwa idadi ya watu wake imeendekea kukua kwa kasi kutoka  milioni 127.4 mwaka 1990 hadi 332 mwaka jana.

Hata hivyo, inakadiriwa kuwa idadi itakua na kufikia watu milioni 560 ifikapo mwaka 2043.

UZALISHAJI BIDHAA 

Rais Ruto anasema kuwa nguzo kuu kwa EAC ni muhimu kuupiga jeki uchumi za mataifa wanachama, kwa kuongeza nafasi za ajira na kufikia malengo ya maendeleo katika ukanda huo.

“Tutalenga kuimarisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa, kuendeleza mpango wa uongezaji wa thamani mazao ya shambani, tutaendeleza biashara miongoni mwa mataifa ya ukanda huu na kuimarisha uwekezaji,” anaahidi.

Mwenyekiti huyo mpya wa EAC anashauri kuwa mataifa wanachama yanapaswa kuondoa vikwazo vya kibiashara baina yao.

“Sharti mataifa ya EAC yaondoe vikwazo kama vile ushuru wa juu kwa bidhaa zinazoingizwa katika nchi wanachama, tuimarishe miundo msingi na tulenge kuoanisha sheria mbalimbali za kibiashara.”

Anasema atahakikisha anaongeza ushindani wa kibiashara, kukuza uzalishaji na uongezaji thamani wa bidhaa za ndani ya jumuiya hiyo.

Aidha, anaeleza vipaumbele kwamba ni kuongeza imani miongoni mwa nchi wanachama na kuimarisha uwekezaji kwa faida ya uchumi EAC. 

"Hivi ndivyo vipaumbele vyangu vya muhimu kwa ajili ya kuleta mageuzi ya uchumi wa EAC, kutengeneza ajira na kuhakikisha kuna maendeleo endelevu kwa nchini zote, amani, usalama na utulivu," anasema.

Anasisitiza pia kusimamia suala la uwajibikaji wa kisiasa na utawala bora kwa kuwa ndiyo njia bora ya kuhakikisha uwapo wa utulivu endelevu katika jumuiya hiyo. 

Rais Ruto, anaongeza kuwa ili kufikia hayo yote ni lazima EAC kuendelea kuimarisha mifumo ya kikanda ambayo inalinda mamlaka yao na usalama wa pamoja, huku akihimiza utawala jumuishi unaoakisi matarajio ya wananchi wa Afrika Mashariki.

"EAC ni jumuiya yenye soko kubwa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu zaidi ya  milioni 300 linalotoa fursa ya kujenga uchumi na kuimarisha biashara kwa manufaa ya watu wa EAC," amesema.

Kadhalika, hakuiweka kando lugha ya Kiswahili kujumishwa na za kimataifa akitaja Kiingereza na Kifaransa, kuwa zitaendelea kutumika EAC, huku akisisitiza  Kiswahili kitabeba utamaduni wa watu wa jumuiya.

ILIKOTOKA EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ya kikanda ya kiutawala inayoanzishwa ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi na utangamano katika Afrika Mashariki.

Chimbuko la EAC lilianzia mwanzoni mwa miaka ya 1900, wakati Kenya, Uganda na Tanganyika (sasa Tanzania) zilipoanzisha uhusiano wa vyama vya ushirika, uliojumuisha Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwaka 1905 na Shirika la Reli na Bandari la Afrika Mashariki 1948. 

EAC ya kwanza ilianzishwa mwaka 1967 na marais wa Kenya, Tanzania na Uganda, hata hivyo, ilivunjwa mwaka 1977 kutokana na kutofautiana kwa sera za kisiasa na kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama. 

Ilirejea upya mwaka 1999, Kenya, Uganda na Tanzania zikianza tena mazungumzo na kusaini mkataba wa kuanzishwa kwake. Mkataba huo ulianza kufanyakazi Julai 2000 na kuanzisha tena EAC. 

Kuhusu wanachama wapya, Rwanda na Burundi zilijiunga na EAC mwaka 2007, Sudan Kusini 2016 wakati  Somalia ilikaribishwa  2024, chombo hicho kikiwa na makao makuu  Arusha, Tanzania.  

Miongoni mwa mafanikio ya EAC ni pamoja na kuwako Umoja wa Forodha ulianza mwaka 2005, ambao hurahisisha usafirishaji wa bidhaa ndani ya kanda, lipo Soko la Pamoja (2010), ambalo hurahisisha kuhamisha watu, wafanyakazi, huduma.

Pia kuwapo mitaji ndani ya kanda Umoja wa Fedha 2013, ambao unalenga kuanzisha sarafu moja, jengo la Taasisi ya Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi, Sauti ya pamoja katika mikutano ya bara na kimataifa.