WATOTO wanne kati ya watano waliookolewa kuozeshwa mkoani Shinyanga, wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, wakipata Daraja B na wawili Daraja C.
Mwenzao mmoja amepata Daraja E katika matokeo hayo yaliyotangazwa juzi na Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania (NECTA).
Watoto hao waliokolewa kwa nyakati tofauti wakiwa wamekatishwa masomo kisha kupelekwa katika kituo cha kusaidia watoto wanaokumbwa na madhila ya namna hiyo cha Agape kilichoko mkoani humo.
Baada ya kufikishwa katika kituo hicho, walirejeshwa shuleni kupitia Waraka wa Elimu Namba 2 wa Mwaka 2021 ulioruhusu wanafunzi wanaokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito, kurejea shuleni.
Utaratibu wa kurejesha wanafunzi hao waliokatisha masomo, ulianzishwa rasmi muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani mwaka 2021 kwa kuagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutengeneza utaratibu maalumu wa kundi hilo kurejea shuleni.
Watoto hao walipelekwa katika Shule ya Msingi Mwapalala, Manispaa ya Shinyanga ili kuendelea kutimiza ndoto zao.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Mlezi wa Kituo cha Agape, John Miyola, alisema amepata faraja kubwa baada ya kuona matokeo ya wasichana hao.
“Kwa kweli nimefarijika sana baada ya kuona matokeo ya wasichana hawa, ni watoto ambao walionekana kukata tamaa sana kutokana na yale waliyopitia, lakini tulipambana kuwarudisha katika mstari mzuri na kuwaambia wasikate tamaa, tunashukuru wanne wamefanya vizuri.
“Nilitamani wote wafaulu lakini haijawa riziki. Huyu mmoja hajafanya vizuri, amepata Daraja E ila hatujamkatia tamaa, tutafanya mpango arudie tena,” alisema.
Miyola alisema kila mwaka anapokea zaidi ya wasichana zaidi ya 50 wanaokimbia kuozeshwa kutoka katika mkoa wa Shinyanga.
Mmoja wa mabinti waliofaulu, mwenye umri wa miaka 15 (jina linahifadhiwa) kutoka katika kijiji cha Rusanda, alisema alikatishwa masomo akiwa darasa la tano mwaka 2020. Alisema aliambiwa anahamishwa kutoka katika mkoa huo kwenda Kigoma kumfuata baba yake mzazi aliyekuwa akiishi huko.
Binti huyo alisema akiwa Shinyanga, alikuwa anaishi na mama yake mzazi ambaye alitengana na baba yake na baadhi ya mahitaji ikiwamo ya shule alikuwa akisaidiwa na mjomba yake.
Alisema baada ya kuambiwa anatakiwa amfuate baba yake, aliahidiwa kuchukuliwa uhamisho katika shule aliyokuwa akisoma awali na alikubaliana na uamuzi huo.
“Lakini cha kushangaza tulipofika Kigoma, mambo hayakuwa kama nilivyoahidiwa. Shule sikuendelea na nilipohoji, niliambiwa uhamisho wangu haukuchukuliwa. Lakini napo sikukaa sana, baba yangu akaniambia kwamba tunatakiwa kurudi tena Shinyanga kwa sababu Kigoma maisha ni magumu.
“Nilifurahi kwa sababu niliamini nikirudi nitaendelea na masomo yangu lakini haikuwa hivyo. Tumerudi ilikuwa mwaka 2021 mwanzoni, nikaomba kurudi kusoma lakini baba akasema haiwezekani kwa sababu tayari nimeshatafutiwa mchumba wa kunioa,” alisema.
Anasema alikataa kwamba hataki kuolewa mpaka akaenda kwa mama yake kumweleza, lakini naye alimwambia kama tayari baba yake amefanya uamuzi huo, hana cha kumsaidia zaidi ya kukubali kwa sababu wako wenzake anaolingana nao wameolewa.
“Mwezi wa tano mwaka 2022 mchumba alikuja nyumbani, nikaitwa nikaenda na babu yangu, wakajitambulisha na wakaniuliza kama ninakubali kuolewa, nikanyamaza. Walivyoona sijajibu hata waliponiuliza mara mbili, mjomba aliniuliza kwa nini sitaki kuolewa napo sikumjibu chochote.
“Mama alimwambia mjomba, huyu hajatakaa tu kusema lakini amekubali, wakati mimi sitaki. Baadaye wakaondoka na mwezi wa sita wakatoa mahali lakini nikakaa mpaka mwezi wa nane ambao ndio ilikuwa harusi,: alisimulia.
Binti huyo alisema wakati sherehe ikiwa ukingoni watu wakitoa zawadi, askari walifika na kumkamata yeye na mama yake wakati huo baba na mjomba wake walipata upenyo na kukimbia lakini baadaye walikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi.
Alisema baada ya mahojiano aliachiwa huru na kukabidhiwa kwa askari wa kike ambaye alimpeleka katika kituo cha Agape.
Binti mwingine mwenye umri wa miaka 16 (jina pia linahifadhiwa) ambaye amefaulu, alisema ametokea Kishapu pia mkoani Shinyanga, alikokuwa akiishi na mama yake, huku baba akiishi wilaya nyingine na mwanamke mwingine.
Alisema akiwa darasa la tatu, maisha yaliaanza kuwa magumu hadi kufikia kwenda kufanyishwa vibarua mashambani na fedha aliyopata ilisaidia mahitaji ya nyumbani kwa sababu mama yao alikuwa mgonjwa.
“Nikiwa darasa la nne, alijitokeza mwanamume kutaka kunioa ambaye alizungumza na mama na shangazi yangu. Nilikataa kuozeshwa kwa nguvu,” alisema.
Alisema licha ya kumshirikisha shangazi ili kumsaidia, alimtaka akubali kwa kigezo kwamba upande wa mwanamume wana mali.
Kutokana na kukosa msaada, alisema alichukua uamuzi mgumu wa kukimbilia mjini ndipo alipowasiliana na dada ambaye aliwahi kufanya kazi kwake na alipomweleza yaliyomsibu, alimsaidia kwa kumkutanisha na mzee mmoja aliyemwunganisha na Agape.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED