Utafiti wabaini uhusiano uelewa wa mtoto darasani na afya ya akili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 12:34 PM Sep 27 2024
Utafiti wabaini uhusiano uelewa  wa mtoto darasani na afya ya akili
Picha:Mtandao
Utafiti wabaini uhusiano uelewa wa mtoto darasani na afya ya akili

UTAFITI umebaini kuwapo kwa uhusiano mkubwa kati ya uelewa darasani na afya ya akili kwa watoto walio katika umri wa madarasa ya awali.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 41 ya watoto wamebainika kuwa na  tatizo la akili, hivyo kushindwa kumudu mbinu za kusoma na kufaulu.

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) Dk. Nabwera Rashid, aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti alioufanya kuhusu  Afya ya Akili ya Watoto wa Shule ya Awali na Uhusiano kwenye Matokeo ya Masomo ya Awali nchini.

 Mhadhiri huyo wa chuo hicho kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),  akizungumza kwa njia ya mtandao kuhusu utafiti huo ulioandaliwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kupitia Jumuiya ya Wadau wa Afya ya Akili Tanzania (TMH-CoP) ECHO, alisema afya ya akili utotoni inahusisha ustawi wa kihisia, kijamii na kisaikolojia wa watoto wenye umri wa miaka sifuri hadi mitano.

 Utafiti alioufanya kwa kuhusisha wilaya tatu za  Arumeru mkoani Arusha, Kinondoni (Dar es Salaam) na Nzega (Tabora), ulihusisha watoto 403 wa umri wa miaka sifuri hadi saba, wakiwamo wa kike ambao ni asilimia 49.6.
 
 Alisema utafiti ulibaini kuwa kati ya watoto hao waliohusishwa kwenye utafiti ambao ni 403, baadhi wakiwa madarasa ya awali kwa madaraja tofauti, ilibainika watoto 169 sawa na asilimia 41, hawako sawa katika afya ya akili, hivyo kuathiri mwenendo wa ujifunzaji.

 Dk. Nabwera alitaja maeneo ambayo watoto hao huathirika zaidi ni katika kuelewa hatua za kusoma kama vile ufahamu wa fonimu, kutaja majina ya picha, ujuzi wa msamiati na ufahamu wa fonetiki.

 “Watoto watundu wanaosababisha matatizo kadhaa 131 ya waliohusishwa kwenye utafiti, hasa nilibaini watoto ni watundu sana yaani hawatulii hata darasani, kwa sababu Dar es Salaam (Kinondoni) ni miongoni mwa mikoa ambayo wazazi, walezi wako ‘bize’ hawana muda wa kulea hawa watoto. Katika kila watoto 10 unaokutana nao njiani watatu hadi watano, wana tatizo la akili.

 Matokeo yalionesha kuwa asilimia 58 ambao ni sawa na watoto 235 wa shule ya awali, walikuwa na alama chini ya wastani katika mtihani wa ujuzi wa kusoma  Kiswahili.

“Hii ina maana kwamba watoto wengi wa shule ya awali, hawakuwa na ujuzi wa kutaja alfabeti, sauti za alfabeti, kusoma na kuelewa, kushika na kufungua vitabu, utambulisho wa barua, majina ya picha na kadhalika.
 
 “Mara nyingi mijadala huhusu afya ya akili inahusu vijana, sasa huu utafiti melenga watoto. Umri huu mtoto hujaribu ku-handle hisia zake na masuala mengine ya kijamii. Huu ndio umri wa kuanza shule, kuna haja ya watoto wa umri huo, kufuatiliwa uweao wao wa uelewa, kuhusiana na jamii nkwa kuwa nao afya ya akili huathiriwa.
 
 Watoto wengi umri huu, ndio wanaingia elimu ya awali, wanafundishwa kusalimia, kuwa na marafiki, kunawa mikono na aseme asante, au samahani na asipopata  elimu hii ndio utakutana na watu ukubwani yeye hana hisia zozote za shukrani, kuomba radhi wala huzuni,” alisema.

 Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 2.8 watoto wa umri huo wako darasani kwa madaraja tofauti kuanzia elimu ya awali. Katika kila darasa, watoto 10 hadi watano wana tatizo la akili.

 “Uchokozi, wizi, uongo, hasira hadi anajipiga chini, nyuma yake kuna tatizo la akili na mzazi au jamii bado hajatambua. Labda akiwa darasani unamwambia nenda mbele kasome au nenda kalale hatekelezi ujue kuna shida. 

“Utakuta mtoto anamaliza kula anatupa sahani hadi inavunjika au akila hapeleki sahani inakotakiwa, ujue kuna shida. Anayefanya vizuri ujue ameshaanza kujua ‘social interactions’ kwamba huyu mkubwa, huyu mdogo,” alibainisha.

 Mhadhiri huyo alisema mtoto aliye na afya ya akili duni akiwa katika umri wa chini ya miaka mitano, akifikia umri wa miaka 14 tatizo litakua.

 “Kwa Dar es Salaam, tatizo la watoto watundu ni kubwa kwa  sababu wazazi wanakimbizana kutafuta maisha. Hii inaweza  kuathiri jamii ya kesho, hawa ndio wazazi na wanajamii wajao miaka 10 hadi 20 ijayo,”alisema Dk. Nabwera.
 
 Alisema elimu ya afya kwa watoto hao ni muhimu kutokana na watoto kujumuisha theluthi moja ya watu wote duniani na asilimia 40 kati yao wanaishi barani Afrika, kwa mujibu wa  Shirika la Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa mwaka 2022.

 Shirika la Afya duniani (WHO) linakadiria kuwa asilimia 10 hadi 20 ya watoto na vijana hupata changamoto ya akili kwa maana kwamba katika kila watoto 10 kutoka miaka mitatu hadi 12, watatu hadi watano wana tatizo la akili huku zaidi ya asilimia 90 ya kesi hizo zikitokea katika nchi za kipato cha chini na kati kama Tanzania.

 Nchini Tanzania, ni asilimia 2.8 tu ya watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi sita wanahudhuria shule ya awali, kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) ya mwaka 2020.

 Takwimu za hivi karibuni kimataifa, zinaonesha katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, takribani watoto milioni 202 wenye umri wa miaka minne hadi 14 hawawezi kusoma kwa ustadi baada ya kuhitimu.

 Nchini Tanzania ni asilimia 12 tu ya wanafunzi wa darasa la pili wanaokidhi viwango vya ufasaha vya kitaifa vya usomaji wa sauti 50 kwa dakika katika Kiswahili.