TAKUKURU yachota mbinu za kimataifa China kukabili rushwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:17 PM Sep 27 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeshiriki Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Ushirikiano katika Mapambano dhidi ya Rushwa (GlobE Network) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na mamlaka hizo.

Mkutano huo uliofanyika China, ni mahususi kwa ajili ya Mamlaka za Kuzuia na Kupambana Rushwa Duniani kubadilishana uzoefu na utaalamu katika jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.

 Mkutano huo wa siku tano umehudhuriwa na Mamlaka 219 za Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoka nchi 121 duniani, ikiwamo Tanzania ambayo TAKUKURU imeshiriki. 

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umehusisha warsha ya Wakuu wa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana Rushwa kutoa uzoefu wao wa namna serikali zinavyofanikiwa kudhibiti rushwa katika mataifa yao.

Kupitia warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila ametoa uzoefu wa namna ambavyo Mfumo wa Sheria na Kitaasisi Tanzania unawezesha mapambano dhidi ya rushwa kufanikiwa. 

Mkurugenzi Mkuu alisema katika warsha kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa inapambana na rushwa kwa kuimarisha mifumo ya sheria na ya kitaasisi, ikiwamo kuanzishwa kwa Divisheni ya Mahakama Kuu inayoshughulikia masuala ya rushwa na uhujumu uchumi, maarufu Mahakama ya Mafisadi. 

Tanzania ni kati ya Nchi 70 zilizopewa fursa ya kutoa wasilisho huko Beijing, China kuanzia Septemba 24 hadi leo ambapo pamoja na mambo mengine amewasilisha mada kuhusu 'Mfumo wa Sheria wa Tanzania kwenye Mapambano dhidi ya Rushwa'. 

Pia alitumia mkutano huu kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa baadhi ya Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa wanaoshiriki Mkutano wa GlobE Network kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya TAKUKURU na mamlaka hizo. 

Viongozi aliokutana nao ni kutoka National Commission of Supervision ya China - Beijing (NCS), Independent Commission Against Corruption (ICAC) ya China - Hong Kong na National Prosecutions Authority (NPA) ya Afrika Kusini. 

Mazungumzo ya Mkurugenzi Mkuu na viongozi hao yalilenga maeneo ya mafunzo ya uchunguzi, ufuatiliaji na urejeshwa mali, ushahidi wa kiuchunguzi wa kina, intelijensia, uzuiaji rushwa, uelimishaji umme, vitendea kazi pamoja na ziara za mafunzo. 

Baadhi ya washiriki, walipopongeza jitihada za TAKUKURU katika kuzuia na kupambana na rushwa pamoja na ushirikiano walionao kikanda na kimataifa na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo. 

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU pia alimtembelea Balozi wa Tanzania China, Khamis Mussa Omar Septemba 23, 2024 kwa lengo la kujitambulisha. 

Akimkaribisha Mkurugenzi Mkuu, Balozi Omar alipongeza TAKUKURU kwa jitihada inazozifanya katika kuzuia na kupambana na rushwa na kusisitiza taasisi hiyo kutumia vyema fursa ya ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Tanzania na ya China kwa kuwa kuna mambo mengi ya kujifunza.