Polisi hatutasubiri moto ilhali moshi unafuka uvunjifu amani

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:46 AM Sep 27 2024
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime
Picha: Mtandao
Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime

JESHI la Polisi nchini limesema kamwe halitasubiri kuona moto ndipo lichukue hatua ilhali moshi unafuka kuashiria vitendo vya uvunjifu wa amani.

Limesisitiza kwamba litaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mtu, watu au kikundi cha watu, kiongozi wa chama cha siasa au wafuasi wao wanaopanga, wanaohamasisha au wanaotenda vitendo vya kihalifu vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Kauli hiyo imetolea baada ya watu na makundi mbalimbali, akiwamo Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Boniphace Mwabukusi, kusema kuwa Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kuzuia maandamano ya vyama vya siasa.

Wadau hao wamesema wajibu wa jeshi hilo ni kuyasimamia na kuyasindikiza kuhakikisha kuwa yanafanyika kikamilifu.

Akijibu hoja hiyo jana, Msemaji wa Jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime alisema: "Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 5 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi kama ilivyorejewa mwaka 2002, ikiwamo kulinda amani ya nchi."

DCP Misime alisema katika maoni ya wadau hao, wametaja vifungu vya sheria ikiwamo vifungu vya 11 (7) na (8) vya Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019.

Alisema kuwa wadau hao wamesema Jeshi la Polisi limeshindwa kutoa sababu za kisheria za kuzuia maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

"Kwamba limeshindwa kusema ni lini maandamano yanaweza kufanyika baada ya zuio na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi halikutakiwa kuingilia masuala ya vyama vya siasa kwa sababu wajibu huo upo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

"Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura 258, kifungu cha 11 (7) (c), inaeleza kuwa endapo mkutano au maandamano yanaonesha au yamedhamiriwa kusababisha uvunjifu wa amani au kuathiri usalama wa umma katika eneo hilo, Mkuu wa Polisi ambaye amepokea taarifa ya mkutano au maandamano hayo atatoa zuio la kufanyika kwa mkutano au maandamano hayo kwa mujibu wa kifungu cha 11 (6) cha sheria hiyo.

"Kifungu cha 11 (8) cha Sheria ya Vyama vya Siasa kinasema ni sharti zuio liwe kwa maandishi na litoe sababu za zuio hilo," alisema.

DCP Misime alisema kuwa katika kutekeleza kifungu hicho, sharti la kutoa sababu za kuzuia maandamano hayo lilitekelezwa na maofisa ambao walipokea taarifa za kufanya maandamano na sababu zilizoainishwa ni pamoja na matamshi kutoka kwa viongozi na wafuasi wa chama kilichowasilisha taarifa ambayo yalikuwa na viashiria vya wazi vya kuvuruga amani ya nchi.

"Kuhusu kutoa taarifa ya lini maandamano hayo yafanyike, sheria haimlazimishi Mkuu wa Polisi anayetoa zuio kueleza ni lini mkutano au maandamano yaliyozuiwa yanaweza kufanyika," alidai.

Alisema kuwa mujibu wa Katiba Sura ya 2 ya mwaka 1977 ibara ya 20 (1) ikisomwa pamoja na Sheria ya Vyama Vya Siasa Kifungu cha 11(1)(a) na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, Kifungu cha 43 (1) (a), (b) na (c), vinatoa haki ya kufanya mikutano au maandamano katika eneo lolote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, DCP Misime alisema pamoja na sheria hizo, Jeshi la Polisi linawaelimisha wananchi kuwa ili kuelewa vyema masuala ya kisheria ni vyema kusoma sheria husika sambamba na sheria zingine zinazohusiana na jambo husika.

"Pamoja na haki zilizotolewa na Katiba na sheria zingine, watambue kuwa hakuna haki isiyokuwa na wajibu kama inavyoainishwa na Ibara ya 30 ya Katiba Sura ya 2 ya mwaka 1977, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 11(6) na (7) cha Sheria ya Vyama vya Siasa na Kifungu cha 43 (3) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, ambazo zinatoa mipaka kwa haki na uhuru na hifadhi kwa haki na wajibu," alisema.

DCP Misime aliwataka wananchi kufahamu kuwa sheria hiyo imeeleza endapo chama cha siasa kitawasilisha taarifa ya kufanya mkutano au maandamano na Ofisa wa Polisi wa eneo husika akawaandikia barua ya kuzuia mkutano au maandamano hayo, kwa mujibu wa Kifungu cha 43(6) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi, kinaelekeza chama husika kukata rufani kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi," alisema.