Mwili askari wakutwa msituni baada ya kupotea kwa siku 50

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 05:37 AM Sep 29 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Daniel Shillah.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Daniel Shillah.

ASKARI wa kikosi cha Valantia (KVZ) Makao Makuu Mtoni, Zanzibar, Sajini Haji Machano Mohamedi, ambaye alitoweka kambini kwa siku 50 wakati wa mazoezi, mwili wake umekutwa msituni ukiwa umeharibika.

Askari huyo alitoweka kambini tangu Agosti 8, mwaka huu, na taarifa ilitolewa katika Kituo cha Polisi Dunga, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja siku iliyofuata.

Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Daniel Shillah, ilisema askari huyo alikuwa akihudhuria mafunzo ya uongozi katika chuo cha uongozi Jeshi la Kujenga Uchumi Dunga.

“Agosti 8, mwaka huu, majira ya saa 8:00 mchana katika msitu ulioko karibu na chuo hicho, askari huyo akiwa na wenzake katika mafunzo alipotea katika mazingira ambayo hayakueleweka.

“Baada ya wenzake kurejea kambini ndipo alipobainika alikuwa haonekani ndipo taarifa hizo zilipelekwa polisi na uchunguzi kuendelea,” alisema SACP Shillah.

Alisema Septemba 26, mwaka huu, saa 10:00 alasiri kwenye msitu ulioko karibu na kambi ya chuo hicho, ulionekana mwili wa binadamu ukiwa umeharibika vibaya.

“Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ulibaini mwili huo ukiwa na nguo na viatu ambavyo zinafanana na zile alizovaa askari huyo siku aliyopotea,” alisema.

SACP Shillah alisema katika mfuko wa suruali aliyokuwa amevaa askari huyo ilipatikana simu ambayo imetambulia kuwa ni yake aliyokuwa akiitumia.

Alisema uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea ukiwamo Ulinganisho wa Vinasaba (DNA) kwa madhumuni ya kubaini ni kitu gani kilichomkuta hadi kusababisha kupoteza maisha ili hatua nyingine za kisheria zifuate.