Milima miwili yaporomoka

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:06 AM Apr 15 2024
Moja ya nyumba za wakazi wa Kata ya Itezi, jijini Mbeya, ikiwa imezingirwa tope baada ya Mlima Kawetere, kumeguka na kusababisha maporomoko tope lililofunika zaidi ya nyumba 20 na shule.
PICHA: NEBART MSOKWA
Moja ya nyumba za wakazi wa Kata ya Itezi, jijini Mbeya, ikiwa imezingirwa tope baada ya Mlima Kawetere, kumeguka na kusababisha maporomoko tope lililofunika zaidi ya nyumba 20 na shule.

ZAIDI ya watu 58 wamefariki dunia katika matukio tofauti ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, huku milima miwili ikiporomoka na kusababisha madhara katika mikoa ya Njombe na Mbeya.

Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema vifo hivyo ni katika mikoa ya Arusha (10), Dar es Salaam (2), Geita (4),  Iringa (5), Kilimanjaro (1), Lindi (4), Mbeya (6), Morogoro (5), Pwani (11) na Rukwa (10). 

Alisema maafa makubwa zaidi yako mkoani Pwani katika Wilaya ya Rufiji na Kibiti ambako kata 17 (12 za Rufiji na tano za Kibiti) zimeathiriwa zaidi.

Alisema Morogoro kuna kata 50 zilizoathirika (Malinyi kata nane, Mlimba tisa, Ulanga nane, Ifakara tisa na Halmashauri ya Mkoa Morogoro kata 22.

Matinyi alisema nyumba zilizoathirika katika mikoa hiyo miwili ya Pwani na Morogoro ni 8,532; Pwani nyumba 628 na Morogoro nyumba 7,904 pamoja na mashamba yenye ukubwa wa jumla ya ekari 76,698 (Morogoro ekari 34,970 na Pwani ekari 41,728).

Alisema zilizoathirika katika maafa hayo kwa ujumla wake ni 10,839 (kaya 4,635 mkoani Pwani na 6,204 mkoani Morogoro).

Pia kuna uharibifu wa miundombinu ya makaravati, madaraja na barabara, hivyo kuathiri huduma za usafiri na usafirishaji na upotevu na mali huku mifugo ikikosa malisho.

Matinyi alisema tayari serikali imechukua hatua mbalimbali na watu waliookolewa ni 2,278. Kati yao, Morogoro ni 78 na Pwani 2,200.

Alisema serikali imeanzisha kambi nane kwa waathirika zenye watu 1,529. Kati yake, saba zina watu 1,394 mkoani Pwani na moja yenye watu 135 mkoani Morogoro ambako wanatoa huduma muhimu zikiwamo za afya.

MBEYA

Wanafunzi 200 wa Shule ya Msingi Generation iliyoko Kata ya Itezi, jijini Mbeya, wamenusurika kifo baada ya mabweni walimokuwa wanalala kufukiwa na tope lililotokana na kuporomoka kwa Mlima Kawetere kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Tope hilo lililoporomoka jana limefunika nyumba 20 za makazi ya wananchi na kusababisha zaidi ya wananchi 200 kukosa makazi, huku dalili zikionyesha mlima huo kuendelea kumeguka.

Tukio hilo lilitokea asubuhi wakati baadhi ya wananchi wakiwa ndani ya nyumba na wengine wakiwa kanisani huku wanafunzi wa Shule ya Generation wakiwa shuleni huko, Waliondolewa kabla mabweni yao hayajafunikwa.

Diwani wa Kata ya Itezi, Sambwee Shitambala alisema tukio hilo limesababishwa na uharibifu wa mazingira kwenye mlima huo hasa ukataji miti ovyo, shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi maeneo ya milimani.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Mbeya, Mrakibu wa Zimamoto, Malumbo Ngata alisema kuwa baada ya kupata taarifa za tukio hilo walikwenda katika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji.

Alisema walianza kuwahamisha watu ambao walikuwa wapo kwenye nyumba zao na kuwapeleka maeneo salama na kwamba hakuna kifo cha mtu yeyote kilichotokea kwenye eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera aliagiza wananchi watakaokosa makazi watafutiwe maeneo salama na masomo yasitishwe katika Shule ya Generation pamoja na ya St. Mary’s ambayo iko jirani.

KILIMANJARO

Jana zaidi ya abiria 1,500 wa safari za usiku na mchana kutoka na kuingia mikoa ya Kanda ya Kaskazini na kwenda mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Dar es Salaam na Morogoro, walisota barabarani kwa saa saba, wakisubiri barabara kuu ya Arusha-Moshi kufunguka, baada ya magogo makubwa, mawe na maji kuifunga kutokana na mvua, Meneja wa TANROADS, Motta Kyando alithibitisha.

KATAVI

Mvua ilioanza kunyesha saa tisa usiku wa kuamkia jana katika Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi ilisababisha watu kushindwa kuendelea na shughuli zao huku abiria waliokua wakisafiri kuelekea mkoani Kigoma na vijiji vilivyoko wilayani Tanganyika wakishindwa kuendelea na safari kutokana na daraja kujaa maji. Diwani wa Misunkumiro, Alfred Matondo alitoa taarifa kuwa zaidi ya nyumba 30 zimezingirwa na maji.

NJOMBE

Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omary, alisema jana kuwa mvua kubwa imesababisha uharibifu wa miundombinu kwa kukatisha mawasiliano kati ya Makete na Ludewa.

Alisema kwenye barabara ya Ikonda –Lupila –Mlangali kuna maparomoko ya udongo ya mlima katika Kijiji cha Masisiwe wilayani Makete na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wakati TANROADS wakufungua eneo hilo ambalo limeonyesha dalili ya maporomoko zaidi.

KIBITI

Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Kanali Joseph Kolombo jana aliomba wadau kujitokeza kusaidia waathirika wa mafuriko ambao nyumba zao zimezingirwa na maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

"Wadau mbalimbali kama taasisi na watu binafsi popote mlipo, ninaomba mwitizame Kibiti kwa jicho la tatu, waathirika hawa wana uhitaji mkubwa, hali si nzuri kwa sasa, misaada ya kibinadamu inahitajika.

"Mpaka sasa tuna jumla ya waathirika 36,900 ambao mbali na nyumba zao kufurika maji, wapo pia waliopoteza mashamba yao," alisema.


 *Imeandikwa na Godfrey Mushi (HAI), Nebart Msokwa (MBEYA), Pilly Kigome (DAR), Neema Hussein (MPANDA) na Julieth Mkireri (KIBITI)