KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla, amesisitiza chama hicho hakitaki mgombea mwenye 'makandokando' ambaye lazima watumie sabuni na dodoki kumsafisha, bali kinataka anayekubalika kwa wananchi.
Amesema chama hicho kamwe hakishindi kwa hila bali kwa haki na kwamba hakihitaji kubebwa, bali utekelezaji ilani yake ni kielelezo kizuri kwa wananchi.
Makalla aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Alisema CCM inahitaji wapigakura milioni 12 kushinda Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwezi Novemba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.
Makalla aliwataka wana CCM kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ili kuwa na sifa ya kuchagua viongozi wa serikali za mitaa.
"Ninawahakikishia kuwa CCM itateua wagombea safi wasio na makandokando. Ninawaagiza viongozi wa chama kuzingatia hili ili kupata wagombea wanaowajibika kwa wananchi.
"Wasiosoma taarifa za mapato na matumizi ya vijiji, uchaguzi ujao hawana nafasi. Jitahidini mchague wenyeviti ambao hawana makandokando, hatutaki mgombea ambaye tumwoshe kwa dodoki na sabuni.
"Tunataka mtu ambaye tukimpeleka kwa wananchi wanamkubali na hakuna minong'ono. Chagueni watu sahihi ambao watatoa matumaini kwa CCM. Chama kinataka uchaguzi wa kishindo na heshima.
"Tusiudharau, tusibweteke, tuweke malengo na mikakati tushinde kwa kishindo. Upo umuhimu na sababu za kushawishi marafiki zetu, wapenda maendeleo watunze imani," alisema Makalla.
Alisema umuhimu wake ni katika mafanikio yote waliyonayo ya utekelezaji ilani kwa amani na utulivu kuanzia wenyeviti wa kitongozi, mitaa, vijiji, madiwani, wabunge na Rais.
Makalla alisema iwapo watakuwa na kiongozi wa upinzani, kuna siku watapeleka maombi ya kujenga madarasa, lakini akasema hakuna eneo la kujenga.
Alijinadi kuwa akiwa wa CCM ataongea na wenzake wa CCM na kutekeleza mradi, ndio maana ni muhimu kuhakikisha wanakiweka chama hicho madarakani.
Kuhusu changamoto zilizoko katika jamii za wafugaji, Makalla alisema serikali inaendelea kuzitatua na mafanikio waliyoyapata ni kutokana na utekelezaji ilani.
"Uhai wa chama chetu ni kuimarisha mabalozi, CCM ina mtaji wa mabalozi, muundo wa CCM ni muundo wa chama imara. CCM inatajwa ni chama namba moja Afrika na namba tisa duniani, sifa hizi ni kutokana na kazi nzuri za mabalozi.
"Ninasimama kifua mbele kuwa msemaji wenu machachari, jeuri yangu ni mabalozi, ndio jeshi kubwa la CCM na jumuiya zake za wanawake, vijana na wazazi,” alisema.
Makalla pia aliomba wana Longido kudumisha amani na umoja kwa kuwa ndio nchi ya mfano yenye makabila mengi 120, lakini hakuna kubaguana.
Alisema walikabidhiwa nchi wakiwa wamoja na hakuna Tanzania nyingine na kila Rais anaahidi kulinda umoja na mshikamano wa nchi.
"Rais Samia anawapenda Watanzania wote, amethibitisha hilo kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.
"Kuna vyama vinataka kutugawa, vinataka faida ya kisiasa kwa kuonesha kabila fulani linabaguliwa, jambo ambalo si kweli.
"Rais Samia anataka umoja na mshikamano wa kujenga Tanzania. Ogopa sana mtu mfitini, msikubali kufitinishwa, wapo wanasiasa wafitini wangependa tusiwe wamoja," alisema Makalla.
Akiwa katika Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Namanga, mkoani Arusha, Makalla alitaka taasisi zote kuongeza kasi ya kuhudumia malori ya mizigo yanayokwenda nchi jirani ya Kenya na kuharakisha biashara baina ya pande zote.
Alisema amefurahishwa na mikakati ya kituo hicho upande wa Tanzania, kuhakikisha malori yanapita katika ukaguzi kwa haraka na kuendelea na safari.
Katibu Mkuu huyo alisema Rais Samia na Rais wa Kenya, William Ruto, wanashirikiana kuhakikisha biashara eneo la mpaka inakuwa rahisi kwa manufaa ya wananchi wote.
"Tuongeze kasi ya kuwezesha mizigo kupita, tuondoe kero ya foleni ya malori, wasikae muda mrefu wanaposubiri ukaguzi, ili kuhakikisha biashara inakwenda kwa wakati," aliagiza.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kali, alisema atasimamia kwa karibu kwa kuondoa kero zote katika mpaka huo ili kuhakikisha biashara inafanyika bila tatizo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED