Makala maalumu: Ana miaka 13 tayari anaitwa mama

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:56 AM Sep 27 2024
Mwandishi wa Nipashe, Elizabeth Zaya akizungumza na mtoto aliyefanyiwa ukatili huo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwandishi wa Nipashe, Elizabeth Zaya akizungumza na mtoto aliyefanyiwa ukatili huo.

NI simulizi ya kuhuzunisha inayomhusu mtoto wa miaka 13 (jina linahifadhiwa), mkazi wa Kishapu, mkoani Shinyanga, akiwasimulia baadhi ya wadau wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) waliofika kwenye kituo anakolelewa.

Katika umri wake wa miaka 13 tayari anaitwa mama baada ya kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mkubwa, kumpa mimba.

Akiwa darasa la sita mwaka jana, mtoto huyo (aliyezalishwa), alifiwa na wazazi wake wote wawili kwa nyakati tofauti akianza baba na kufuatia mama yake.

Kutokana na vifo vya wazazi wake, maisha yalikuwa magumu, ikabidi achukuliwe na mama yake mkubwa akaishi naye na akachukuliwa uhamisho ili akaendelee na masomo yake.

Nyumbani kwa mama yake mkubwa, alikuwa anaishi pia kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake huyo, aliyekuwa na mke na watoto. Alipofika, akawa anaishi nao akijua ni ndugu zake.

Chumba chake cha kulala alilala na binti mwenzake.

Anasema baada ya kukaa siku kadhaa pale nyumbani kwa mama yake mkubwa, maisha hayakuwa mabaya sana awali, lakini baadaye binti aliyekuwa analala naye alisafiri na hapo ndipo maisha yake yalipoanza kuwa 'machungu'.

Kuanzia siku hiyo kaka yake alianza kuingia chumbani kwake na kumwingilia kimwili kwa nguvu huku akimdanganya kumpatia fedha Sh. 500, na kwa kuwa alikuwa hajaizoea sana familia hiyo, aliogopa kumwelezea mtu yeyote madhila aliyokuwa akipitia.

"Kaka aliendelea mara kwa mara kuja chumbani kwangu usiku na kunibaka, alisema nisipige kelele, anasema atanipa Sh. 500. Niliogopa kumwambia hata mama mkubwa, wala mtu yeyote kwa sababu nilikuwa zijawazoea sana.

"Lakini baadaye nilianza kuugua, mama mkubwa aliponipeleka hospitalini wakasema nina mimba na akaniuliza ni ya nani, nikamwambia kaka ndiye alikuwa ananibaka kwa nguvu chumbani kwangu."

Anasimulia kwamba baada ya kupatiwa taarifa hizo kaka yake (aliyempatia ujauzito) alikimbia na hajulikani aliko mpaka sasa.

Baada ya kujulikana kwamba mtoto huyo alifanyiwa ukatili huo na kaka yake nyumbani alikokuwa akiishi, Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga uliamua kumpeleka katika kituo kinachosaidia mabinti na watoto wanaokumbwa na madhila ya namna hiyo kinachojulikana kama Agape Knowledge Open School cha mkoa huo.

"Walivyoniambia nina mimba wakanileta hapa kituoni, ndipo nikaanza kulelewa hapa mpaka sasa nimejifungua mtoto ana miezi minne," anasimulia.

Anasema kwamba, haelewi namna ya kumlea mtoto wake, kwa hiyo mara nyingi amekuwa anasaidiwa na mabinti wengine wanaomzidi umri waliopo katika kituo hicho.

Mtu mwingine anayemsaidia kulea mtoto wake ni mama anayeishi kituoni huko kwa ajili ya kuwasimamia.

Mlezi Mkuu wa Kituo hicho cha Agape, John Miyola, anasema mtoto huyo alifika kituoni kwake mwezi Machi mwaka huu na wakamsaidia kutatua baadhi ya changamoto za kiafya zilizokuwa zinamkabili na akafanikiwa kujifungua mtoto salama.

"Huyu binti alifiwa na wazazi wake wote kwa nyakati tofauti na wa mwisho kufariki alikuwa mama yake, sasa mama yake mkubwa alimchukua kwenda kumlea akiwa darasa la sita.

"Mama mkubwa alikuwa na kijana wake ambaye ana mke na watoto, kwa hiyo akawa akilala usiku anakwenda kumwingilia kimwili kwa nguvu.

"Binti akienda kuchota maji, akitoka shuleni, anamtumia, usiku anamtumia. Sasa ilifika kipindi mtoto akaanza kuugua ikabidi wampeleke hospitalini, na walipofanya vipimo ikagundulika kwamba tayari alikuwa mjamzito.

Anasema baada ya taarifa zile, kila mtu alishikwa na mshangao na hivyo ikabidi wampige simu ili wamhamishie kituoni kwake wakati huo taratibu nyingine za kisheria zikichukuliwa.

"Kwa hiyo ilikuwa ni mshangao mkubwa kwa kila mtu kwa sababu ya umri wenyewe wa mtoto aliyepewa ujauzito, sasa hivi ana miaka 13 kwa maana hiyo wakati anapata ujauzito alikuwa na miaka 12, na kibaya zaidi hata yule kaka yake mwenyewe aliyemsababishia madhila hayo alikimbia, baada ya hapo, hospitalini waliamua kwamba wamlete hapa kituoni," anasema Miyola.

Anasema mtoto huyo alikuwa na changamoto ya damu pungufu, hivyo ilibidi wapambane kumpatia vyakula vya kuongeza damu.

"Katika hali yake hiyo ya ujauzito alikuwa na damu saba tu, kwa hiyo ikabidi tuanze kupambana kumpatia vyakula vya kuongeza damu na tulifanya hivyo mpaka ikawa sawa.

"Tumeishi naye hapa kuanzia Machi mwaka huu mpaka miezi tisa akaenda kujifungua, alipata changamoto kidogo, lakini Mungu ni mwema madaktari walipambana akajifungua salama na mwanawe ana miezi minne sasa," anasema Kata ya Chibe

Miyola anasema changamoto nyingine iliyomtokea mtoto huyo ni kukosa maziwa ya kumnyonyesha mwanawe na kulazimika kununua dukani.

Miyola anakiri kwamba mtoto huyo hana uwezo hata wa kumlea mwanawe, anasaidiwa na timu ya wenzake walioko kituoni.

"Huyu mtoto ni mdogo sana, yeye mwenyewe bado alikuwa anahitaji kulelewa kama ilivyo watoto wengine, kwa hiyo si rahisi ajue kulea, kuna mabinti hapa ni wakubwa kidogo wanamsaidia na wana mama anayewasaidia, kwa ujumla kituo ndio kimechukua jukumu la kulea hicho kichanga, wote ni watoto kwa hiyo wote wanalelewa," anasema Miyola.

Anasema baada ya mtoto kujifungua, walimsaidia akaendelea na masomo na amehitimu darasa la saba mwaka huu, anasubiri matokeo.

Lilian Kimati ni Mratibu wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania, unaounda zaidi ya mashirika 80 ikiwamo la Msichana Initiative, Binti Makini Foundation, Theatre Arts Feminist Group, Medea, Plan International na My Legacy, anawaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia mahitaji mbalimbali katika ulezi wa mtoto wake.

Pia wawasaidie mabinti wengine wanaosaidiwa katika kituo hicho ambao wengi wao wako huko baada ya kukumbwa na madhila mbalimbali zikiwamo mimba na ndoa za utotoni.

Mipawa Ngusa ni Kaimu Mtendaji wa Kata ya Chibe wilayani ya Shinyanga Manispaa, mkoani Shinyanga, kilipo kituo anapolelewa mtoto huyo, anasema wakati anapelekwa kituoni hapo walishirikishwa na alikuwa na hali ya tatizo la afya ya upungufu wa damu, hivyo wakashauri asidiwe.

"Ni kweli tulishuhudia huyu mtoto alipoletwa hapa na baada ya kumwangalia kiafya alikuwa na shida ya damu, lakini alisaidiwa ikakaa sawa mpaka alipojifungua.

"Ni mtoto ambaye anahitaji msaada, kama kuna mashirika ambayo yanaweza kumsaidia tunaomba wajitokeze, si tu kwa huyu mtoto, lakini kwa mabinti wote waliopo katika kituo hiki maana wengi wamekutwa na madhila," anasema Ngusa.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 130 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, ni kosa la jinai kwa mtu mwanamume kumnajisi mtoto na adhabu yake imetajwa katika kifungu cha 131 cha sheria hiyo kuwa ni kifungo cha miaka 30 gerezani.