Majaliwa ataka ushirikiano utekelezaji uchumi jumuishi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:26 AM Sep 27 2024
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Picha:Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kushirikiana kikamilifu na nchi zinazoendelea katika kusaidia utekelezaji wa mifumo jumuishi ya kifedha.

Majaliwa alitoa wito huo juzi wakati akifungua mjadala kuhusu  miaka 15 ya  mafanikio katika Mfumo Jumuishi wa Fedha kwa Maendeleo kwenye mkutano ulioitishwa na Malkia wa Uholanzi, Maxima, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Huduma Jumuishi za Fedha, New York, Marekani. 

Alisema uchumi jumuishi ni muhimu hasa katika utekelezaji wa mpango endelevu wa maendeleo na ufanikishaji wa ajenda 2030.  

 “Huduma jumuishi za kifedha ni kiungo muhimu cha ukuaji wa uchumi, kupunguza umasikini na kuleta maendeleo ya jamii kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu.  

Aidha, Majaliwa alimpongeza Malkia Maxima kwa juhudi ambazo zimewezesha ongezeko kubwa la kufikiwa kwa huduma za kifedha duniani, huku zaidi ya asilimia 50 ya watu wakiwa wamefikiwa na mpango huo katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. 

“Umiliki wa akaunti duniani umeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 76 mwaka 2021. Haya ni mafanikio makubwa lakini changamoto imebaki hasa kwa wanawake waishio katika nchi zinazoendelea. Wengi  wao bado hawajaingizwa kwenye mfumo jumuishi wa kifedha,” alisema. 

Awali, Malkia Maxima alisema anafurahishwa na hatua iliyofikiwa sasa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa hapo awali. 

"Wakati tunaanza hii kazi ya kuhimiza mifumo jumuishi ya kifedha hatukuwa na takwimu zozote. Tulipanda na kufikia asilimia 50 na sasa tunakaribia asilimia 80. Natambua asilimia 80 siyo sawa na asilimia 100, ni lazima nikiri kuwa kazi imefanyika," alisema. 

Akionesha dhahiri kuwa bado kazi haijaisha, Malkia Maxima alisema mkakati uliopo ni kuwafikia watu bilioni 1.5 ambao bado hawajafikiwa na huduma jumuishi za kifedha. 

Alisema anafarijika kuona watu wa rika mbalimbali wakitumia mifumo hii kwenye maeneo ambayo huduma za kifedha zinapatikana.

 "Mabibi wanaweka fedha na kusomesha wajukuu zao, vijana na mabinti wajasiriamali wanatumia huduma hizo kutunza fedha zao, kupata mikopo midogo midogo na kukuza mitaji yao," alisema. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliishukuru serikali ya Marekani kwa misaada inayoipatia Tanzania kupitia  wadau mbalimbali kama Shirika la Misaada ya maendeleo (USAID), Vodafone Foundation, Rockefeller Foundation na Ford Foundation na hasa kwenye masuala ya uchumi, kijamii na utawala bora. 

Alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anashukuru kwa hatua hiyo kwani inaendana na maboresho ambayo serikali yake imeamua kuyatekeleza ili kuleta ujumuishi kwenye jamii  kwa faida ya siku za usoni. 

"Tanzania imedhamiria kuboresha mifumo yake ya kisheria na kuimarisha demokrasia ili kuleta ujumuishi na maendeleo endelevu. Tunatambua kuwa tunapaswa kuunganisha nguvu zetu tunapoamua kukabiliana na changamoto za kidunia kama vile tofauti za kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi na vurugu za kisiasa. Ushirikiano ama ubia kama huu ambao  tunajivunia leo, ndiyo msingi wa  kuleta mabadiliko na maendeleo endelevu," alisema.