Kuelekea Siku ya Moyo Duniani; Ulaji wanga saa chache kabla ya kulala usiku hatari

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 03:52 PM Sep 27 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge (kushoto), akizungumza na moja ya waliofika katika kambi zinazoandaliwa na taasisi hiyo.
Picha:Mpigap
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge (kushoto), akizungumza na moja ya waliofika katika kambi zinazoandaliwa na taasisi hiyo.

ULAJI wa vyakula vyenye wanga hasa saa chache kabla ya mtu kwenda kulala, kunatajwa kuwa hatari kwa afya, hususan Magonjwa Yasiyoambukiza (NCDs), ukiwamo ugonjwa wa moyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge, ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam, kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani.

Siku hiyo ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo Septemba 29, lengo ni kuikumbusha jamii kupima afya angalau mara moja au mbili kwa kipindi kisichopungua miezi 12.

Akifafanua zaidi kuhusu siku hiyo, mbele ya waandishi wa habari, Dk. Kisenge ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo, anasema idadi ya wanaougua maradhi hayo inakua, akisema kauli mbiu mwaka huu: Tumia moyo wako chukua hatua, ujilinde na magonjwa ya moyo na uwasaidie watu wengine.

“Duniani kote takribani watu milioni 17 hupoteza maisha kutokana na magonjwa ya moyo kila mwaka. Kwa nchi yetu tatizo hili limefikia asilimia 13, huchangia vifo vingi hasa vya ghafla. Kuna magonjwa ya mishipa ya damu, valvu na presha.

Vitu vinavyochangia sana magonjwa ya moyo ni pamoja na uvutaji wa sigara, unywaji wa pombe, unene uliokithiri, kutozingatia lishe, kula sukari nyingi na ulaji wa wanga hasa kula wakati umechelewa usiku sana, unachangia unene, hatimaye magonjwa ya NCDs

JKCI tunaadhimisha siku hii, kwa kufanya matembezi Septemba 28, mwaka huu, kwa kuwaambia wananchi kuwa unapofanya mazoezi unapotembea unaepusha magonjwa haya kwa zaidi ya asilimia 10,” amesema Dk. Kisenge.

Amesema pia maadhimisho hayo kwa siku ya pili, Septemba 29, mwaka huu JKCI itatoa huduma bure za vipimo na matibabu kwa wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam, katika kambi itakayofanyika eneo la Kawe.

Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto JKCI, Dk. Sulende Kubhoja alisema upande wa watoto chini ya miaka 18 wengi huugua magonjwa hayo ikiwa ni tangu kuzaliwa kwao, tofauti na watu wazima ambao sababu ni mtindo wa maisha.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Dar Group-JKCI, D. Tulizo Sehemu, amesema viwango vya wagonjwa wanaotibiwa katika tawi hilo la taasisi hiyo kwa siku inafikia wagonjwa 500 hadi 600.