BoT yaongeza riba kwa benki, thamani Shilingi yaporomoka

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:17 AM Apr 05 2024
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.
Picha: Maktaba
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba.

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imepandisha kiwango cha riba ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka asilimia 5.5 hadi sita, ambayo itatumiwa na benki nchini katika robo ya pili ya mwaka huu kuanzia Aprili hadi Juni, huku ikibainisha kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola kutoka asilimia 1.6 mwaka 2023 hadi 1.8.

Uamuzi wa kupandisha riba ya BoT ulifikiwa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Aprili 3, mwaka huu, ambacho kilizingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi iliyofanyika Machi, mwaka huu.

Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa kamati hiyo imeona umuhimu wa kuongeza riba itakayokuwa na wigo wa asilimia mbili ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia.

“Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi nchini licha ya changamoto zilizotokana na mtikisiko katika uchumi wa dunia. Tuna akiba ya kutosha ya fedha za kigeni dola bilioni 5.3 ambayo itawezesha huduma na kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nje kwa miezi minne.

“Thamani ya Shilingi dhidi ya dola pia ilipungua kwa asilimia 1.8 katika robo ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na asilimia 1.6 katika robo ya mwisho ya mwaka 2023. Hali hii ilitokana na msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni pamoja na mazingira ya kiuchumi duniani,” alisema Tutuba.

Aidha, alisema kamati hiyo pia ilijadili kuhusu upungufu wa fedha za kigeni nchini na kujiridhisha kwamba hatua za kuongeza upatikanaji na kupunguza matumizi ya dola zinazotekelezwa sasa zinatarajiwa kupunguza changamoto hiyo ndani ya muda mfupi ujao.

Hata hivyo, alisema sekta ya kibenki imeendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha, ikiendelea kutengeneza faida na  ubora wa rasilimali za benki ukiendelea kuridhisha, huku uwiano wa mikopo chechefu ukiwa ni asilimia 4.3 ambayo iko ndani ya wigo unaokubalika wa uwiano wa chini ya asilimia tano ya mikopo yote.

Mwenyekiti wa Umoja wa Benki Tanzania (TBA), Theobald Sabi, alisema riba hiyo ni lazima kuiangalia kwa muktadha wa kiuchumi, akieleza kuwa viwango vya mikopo chechefu vimeendelea kushuka hadi asilimia 4.5 katika soko zima la kibenki.

“Benki zina ukwasi wa kutosha hivyo wananchi wategemee kwamba mikopo itaendelea kupatikana na benki zinachukua hatua kuhakikisha kwamba mikopo inapatikana kwa mashariti rafiki kwa waliowengi,” alisema Sabi.