Zanzibar yaongeza bajeti elimu ya juu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:49 AM Sep 29 2024
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi,Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mtandao
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi,Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeongeza bajeti ya elimu ili kuwawezesha vijana zaidi kunufaika na mikopo na kuendelea na elimu ya juu.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliyasema hayo jana Tunguu, wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja kwenye Mahafali ya Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu Zanzibar, yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana (UVCCM) katika ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar  (SUZA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano Ikulu, Zanzibar, Rais Mwinyi alisema serikali imeongeza bajeti ya elimu kutoka Sh. bilioni 265.5 kwa mwaka 2021/22 hadi Sh. bilioni 851 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 221. 

Dk. Mwinyi aliwahakikishia vijana wote wanaopata fursa ya kujiunga na elimu ya juu kuwa watapata mikopo isiyo na masharti na kusema serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar kutoka Sh. bilioni 4.0 mwaka 2011 hadi Sh. bilioni 33.50 mwaka 2024.

Alibainisha kwamba kiwango hicho cha fedha kinawasomeshea vijana 7,367 wa elimu ya juu kwa kuwanufaisha wanaosoma vyuo vya ndani na nje ya Tanzania.

Dk. Mwinyi alisema ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wananufaika na fedha hizo, tayari serikali imeanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma ngazi za stashahada.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwaelezea wanafunzi 365 wenye ufaulu bora zaidi wa daraja la kwanza wananufaika na ufadhili unaotolewa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini.

Kadhalika, alisema serikali imeimarisha mafunzo ya amali kwa kujenga miundombinu imara ya fani za ufundi wa aina tofauti inayofundishwa kwa vyuo vya mafunzo ya amali nchini ili kuwajenga kiuweledi wahitimu wa vyuo hivyo wanapomaliza masomo yao wajiajiri na kuajiriwa.

Aliwataka vijana kutumia fursa ya elimu iliyopo kwa kujiendeleza pamoja na kuongeza maarifa ya kitaalmu waliyoyapata kipindi cha mafunzo yao.

Kuhusu ujenzi wa vyo vikuu, Rais Dk. Mwinyi alisema tayari serikali imeanza ujenzi wa vyuo vyengine vipya vitano vya mafunzo ya amali Unguja na Pemba ili kutoa fursa zaidi kwa vijana wengi kupata ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira. 

Alisema ujenzi wa vyuo hivyo ni jitihada za serikali anayoiongoza za kuimarisha uwekezaji kwenye huduma za jamii na ujenzi wa miundombinu ikiwamo ya barabara, viwanja vya ndege, bandari, masoko na kuhamasisha wawekezaji wa sekta ya utalii na ujenzi wa viwanda, ni miongoni mwa dhamira za kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa nchi. 

Kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake hususan kwenye ajira, Dk. Mwinyi amebainisha miradi 330 yenye mtaji wa dola za Marekani bilioni 5.4 imesajiliwa na kutegemewa kuzalisha zaidi ya ajira 18,000 kwenye uwekezaji na shughuli za biashara. 

Alisema juhudi hizo zinakwenda sambamba na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi wakiwamo vijana kupitia “Programu ya Inuka” na serikali iliweka Sh. bilioni 15 za mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa kwa wananchi.