WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, ameipongeza Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa jitihada za kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Pia amesisitiza kuwa juhudi hizo ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutekeleza falsafa ya 4R inayojikita katika Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na na Kujenga Upya Taifa.
Waziri Chana aliyasema hayo jana wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za TTB, jijini Dar es Salaam.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuitangaza nchi lakini nasisitiza lazima muwe na ushirikiano katika taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili twende kwa pamoja. Mwende uwandani na kuvijua vivutio vilivyoko katika taasisi zote,” alisema.
Waziri pia aliweka bayana kuwa serikali inaitegemea bodi hiyo kuendelea kuingiza mapato hasa fedha za kigeni na kuitaka kutengeneza programu endelevu za muda mrefu za kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi na kuhakikisha utafiti wa utalii unaotolewa unajulikana kwa taasisi zingine za serikali zikiwamo bunge na vyuo vikuu.
Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, alisema bodi hiyo imejikita katika vipaumbele kadhaa ikiwamo kuhakikisha uendelevu wa kifedha wa taasisi hiyo kwa kuwekeza kwenye mali za TTB na kuzalisha mapato kupitia Kituo cha Kutangaza Utalii Kidijitali (DDMCC).
Pia alisema TTB itajikita katika kutengeneza mgawanyiko wa kikanda wa maeneo ya vivutio vya utalii na kubuni mazao mapya ya utalii kama ‘Boat Cruises’ sambamba na mbinu mpya za kutangaza utalii pamoja na kushawishi waendeshaji wa biashara ya utalii kuhusu namna bora ya kuandaa vifurushi vya utalii ili kupata wageni wengi zaidi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED