NCHI 12 kutoka Afrika, Ulaya na Marekani zinakutana jijini Dar es Salaam kujadili namna ya kupata teknolojia rahisi mbadala wa matumizi ya zebaki kwenye shughuli za uchimbaji madini ili kukomesha matumizi ya kemikali hiyo.
Mkutano huo wa siku nne ulifunguliwa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Cyprian Luhemeja, ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Dk. Ashatu Kijaji.
Baadhi ya nchi zinazoshiriki mkutano huo ni pamoja na Tanzania, Zambia, Kenya, Senegal Ghana, Bukinafaso, Austaralia, Ujerumani, Marekani na Colombia.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo, Luhemeja amesema lengo la mkutano huo ni kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu wa teknolojia mbadala ambazo zinatumiwa na wachimbaji wadogo kwenye uchimbaji wa dhahabu.
Amesema kuna baadhi ya nchi kama Ghama ambazo zimeanza kuondokana na matumizi ya zebaki kabisa baada ya kubaini teknollojia mpya mbadala ambayo inapendwa na wachimbaji.
Luhemeja amesema lengo la serikali ni kuhakikisha inafanya jitihada kubwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo na kuingiza teknolojia mbadala ili ifikapo mwaka 2030 kusiwepo na matumizi ya zebaki hapa nchini.
Alisema matumizi ya zebaki yamekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madhara kwa afya ya binadamu na viumbe hai kwenye maeneo ambayo imekuwa ikitumika.
Amesema nchi nyingi duniani zinapunguza matumizi ya zebaki kwasababu inakaa kwenye ardhi kwa muda mrefu na imekuwa ikichafua hali ya hewa na kusababisha athari nyingi.
Amesema Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limekuwa na mikakati mbalimbali ya kutokomeza matumizi ya zebaki naa kwamba mkutano huo utawapa uzoefu na mbinu zinazotumiwa na mataifa mbalimbali.
Amesema inakadiriwa kuwa nchini Tanzania zinatumika tani 21,000 za zebaki katika shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwenye mikoa mingi nchini ikiwemo Mbeya na Singida.
Amesema serikali kwa sasa inamradi mkubwa kwenye mikoa tisa lengo la mradi ikiwa ni kuwafundisha wachimbaji wadogo wadogo namna ya kuachana na matumizi ya zebaki.
Amesema serikali inajenga kituo Msalala Shinyanga ambacho kitakuwa sehemu ya mafunzo kwa wachimbaji wadogo kuhusu namna ya kutumia teknolojia mbadala kwenye shughuli zao za uchimbaji wa madini.
“Kupitia maonyesho ambayo tumeona kwenye mkutano huu tumeona teknolojia mbalimbali rahisi na nafuu ambazo zitatumika kwenye uchimbaji wa madini na lengo la serikali ni kuachana na maatumizi ya zebaki ndani ya miaka 10 ijayo kama malengo ya milenia yanavyotaka,” amesema Luhemeja.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, amesema ugeni huo kutoka mataifa mbalimbali duniani ni fursa kubwa kwa watanzania kupata uzoefu wa namna ya kuondokana na matumizi ya zebaki katika uchimbaji mdogo wa dhahabu.
Amesema NEMC itatumia mkutano huo kuangaliaa teknolojia gani rahisi, nyepesi na rafiki kwa mazingira zinazotumiwa na mataifa mengine yaliyofanikiwa kuachana na matumizi ya zebaki na kisha kuwaelimisha wachimbaji wa Tanzania kuzitumia.
“Matumizi ya zebaki yamekuwa yakisababisha madhara makubwa kwa afya ya binadamu, viumbe hai na mazingira na kwa bahati mbaya zebaki ni madini ambayo yakiingia kwenye maji au kwenye mwili na kwenye mifumo ya kiikolojia hayatoki,” amesema Dk. Semesi
“Tutatumia mkutano huu kupeana ujuzi na teknolojia mbadala na jinsi ya kutoa elimu kwa wachimbaji wetu ili mpaka kufikia 2030 tuwe tumeshaondokana kabisa na matumzi ya zebaki kama wenzetu walivyofanikiwa,” amesema Dk. Semesi.
Amesema Mfuko wa Mazingira (GEF) unafadhili nchi zita Afrika, Tanzania ikiwa moja wapo ili zipambane na matumizi ya zebaki kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED