Mwinyi aonesha utayari ushirikiano na shirika la uendeshaji bandari Indonesia

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 07:08 AM Sep 07 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mtandao
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali iko tayari kushirikiana na Shirika la Pelindo kujenga Bandari Jumuishi ya Mangapwani ambayo itajumuisha sehemu ya kuhifadhi nafaka, makontena, bandari kavu, chelezo na hifadhi ya mafuta.

Pia bandari hiyo inatarajiwa kuwa kituo cha kuhudumia eneo la ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika. 

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana alipotembelea Bandari ya Tanjung Priok, Jakarta nchini Indonesia na  kukutana na uongozi wa Pelindo, shirika  linalomilikiwa na serikali ya nchi hiyo ambalo linaendesha shughuli zote za bandari nchini humo.

Rais Dk. Mwinyi alisema anatambua kuwa Indonesia na Zanzibar zinafanana kwa kuwa ni nchi za visiwa na hutegemea bahari kwa shughuli za uchukuzi.

Pia alisema muundo huo wa kijiografia wa visiwa una changamoto mbalimbali za usafirishaji, hivyo bandari inachukua nafasi muhimu katika kutatua changamoto za kibiashara na kuchochea kukua kwa uchumi wa nchi.

Arif Suhartono, Mkurugenzi Mkuu wa Pelindo yenye matawi 71 nchini humo, ikijumuisha kisiwa cha Sumatra kwa upande wa magharibi hadi mashariki ya Papua New Guinea, alisema ziara hiyo iwe mwanzo wa ushirikiano wa karibu zaidi na kuweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Indonesia na Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi amekamilisha ziara yake nchini humo iliyoanzia Septemba Mosi hadi 3, mwaka huu, katika kisiwa cha Bali. 

Dk. Mwinyi alimwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika.