"Kiama cha mafisadi kwenye korosho, ufuta na mbaazi Kusini kinakuja"-Ado

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:58 AM Sep 12 2024
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kuwa kinafuatilia kwa karibu na kuchunguza vitendo vya ufisadi katika usambazaji wa pembejeo za kilimo na masoko ya mazao ya korosho, mbaazi na ufuta katika mikoa ya Ruvuma, Tunduru na Ruvuma.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alisema; "Juzi nilikuwa Tunduru na leo nipo Nanyumbu na Masasi, kilio ni kilekile. Wakulima wanapunjwa pembejeo na kuna wizi mkubwa kwenye minada ya korosho, mbaazi na ufuta" alisema na kuongeza;

"ACT Wazalendo tunafuatilia kwa karibu malalamiko haya. Tunataka tuwajue hao wezi wa pembejeo na watu wanaohujumu minada ya korosho, mbaazi na ufuta. Tukiwapata, tutawataja hadharani. Tumejitoa mhanga kwa kazi hii. Tutatoa orodha ya Mafisadi katika mnyororo wa thamani katika mazao ya mbaazi, korosho na ufuta Kusini" alisema Ado.

Katika hatua nyingine, Ado alisema kuwa Chama cha ACT Wazalendo kinaupinga mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu umeshindwa kumkomboa mkulima kwa kumwezesha kupata pembejeo bure na kwa wakati  na malipo ya mazao kwa uhakika na bei nzuri. "ACT Wazalendo inataka wakulima walipwe papo kwa papo wanapouza mazao yao" alisisitiza Ado.

Ziara ya Ado Shaibu katika Mikoa ya Kusini na Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa inaingia siku ya pili ambapo anatarajiwa kufanya vikao vya ndani na mikutano ya hadhara kwenye majimbo ya Ndanda na Mtwara Vijijini.