Dk. Mwinyi aanika mikakati ukuaji uchumi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:53 PM Nov 23 2024
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mpigapicha Wetu
RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amebainisha mikakati ya serikali kuhusu ukuaji uchumi wa Zanzibar na kueleza kuwa inaendelea kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wote wanaotumia bandari ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi amesema hayo jana alipozindua, kutia saini na kushuhudia utiaji wa saini Mpango wa Maboresho ya Utoaji Huduma kwa Bandari ya Zanzibar (Zanzibar Port Improvement Charter).

Utoaji huo wa huduma ni kwa ushirikiano wa serikali, wadau wa bandari kutoka taasisi za umma na binafsi pamoja na Taasisi ya Tony Blair (TBI).

Alisema lengo la mpango huo ni kuondosha usumbufu kwa kupeana majukumu kwa kila mdau, kupitia viashiria vilivyoandaliwa ndani ya mpango huo sambamba na kurahisisha ushushaji wa makontena (makasha).

Pia ukaaji wa meli ukutani, kusubiria ukuta pamoja na masuala ya ‘Customes Clearance’ kwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za bandari ili kutoa msukumo wa ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kuhusu upakiaji na ushushaji wa makontena bandarini, Rais Mwinyi amewahakikishia wafanyabiasha wa Zanzibar kwamba, serikali imedhamiria kwa dhati kuimarisha utoaji wa huduma kwa kurahisisha mchakato huo katika bandari zote nchini.

Alisema hatua hiyo ni kwa mujibu wa wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 hadi 2025 katika Ibara ya 167(b) inayozungumzia kuimarisha huduma za bandari kwa kutumia vifaa na teknolojia za kisasa.

Lengo la kufanya hivyo, alisema ni kuongeza idadi ya makontena kutoka 82,312 mwaka 2018 hadi 105,000 ifikapo 2025 na kupunguza siku za kuegesha meli kutoka siku saba mwaka 2018 hadi siku tano mwaka 2025.

Alisema kwa sasa uwezo wa bandari za makasha tatu; Malindi, Fumba na mkoani Pemba zina uwezo wa kuhudumia makasha zaidi ya 105,000.

Rais Mwinyi alisema makubaliano hayo baina ya serikali na taasisi hizo ni utekelezaji na ufanisi kwa Bandari ya Zanzibar pia, kutafanyika upimaji wa kila kilichotekelezwa na taasisi hizo kila inapotimia mwaka mmoja.

Alisema endapo taasisi zote zitatekeleza wajibu wao ipasavyo, mafanikio makubwa yatapatikana nchini, akitolea mfano nchi za Singapore, Mombasa-Kenya, Gambia kwa kufanikiwa na mpango kama huo wa utoaji huduma wa bandari ambao wamepiga hatua kubwa ya mafanikio.

Katika hatua nyingine ya kuboresha huduma za bandari Rais Mwinyi alisema, serikali inatarajia kuanza ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani inayotarajiwa kuhudumia meli kubwa za mafuta na gesi.

Alisema ujenzi wa bandari hiyo unakwenda sambasamba na Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM, kifungu 167(c) kinachoielekeza serikali kujenga miundombinu ya kuhudumia meli zinazopita mwambao wa Afrika Mashariki, kupata huduma za kuongeza mafuta, maji safi na kufanya matengenezo.

Rais Mwinyi aliwataka wadau wa bandari ya Zanzibar ikiwamo Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi yenye kubeba jukumu kubwa la taifa la kusimamia miundombinu nchini.

Kadhalika alisema kuendelea kuwa karibu na watumiaji wa miundombinu hiyo kwa kuwapelekea huduma na nyenzo ili kuhakikisha wananchi wanatumia miundombinu bora na yenye tija kwa ustawi wa jamii na kuinua uchumi wa Zanzibar kwa maendeleo ya wananchi.

Rais Mwinyi alisema jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi wanashirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza sekta ya Uchukuzi.

Aliwaomba wafanyabiashara waendelee kufanya kazi zao kwa uaminifu, maadili na uzalendo ili kujipatia kipato halali na kuzingatia wajibu wao wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Waziri Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed alisema kusainiwa kwa mpango huo ni makubaliano baina ya serikali na wadau wa bandari hiyo zikiwamo taasisi za umma na binafsi kufanyakazi kwa pamoja ili kuongeza ufanisi na kuleta tija katika kukuza Uchumi wa nchi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Akif Ali Khamis alipongeza hatua ya serikali kuleta mapinduzi makubwa kwa sekta ya bandari ya Zanzibar kuhusu uendeshaji wa bandari hiyo baada ya kuingia mkataba na Kampuni za Zanzibar Multiple, kampuni ya Bandari ya Fumba na ya Mkoani kwaajili ya kushusia makasha (makontena.

Kiongozi wa timu ya Taasisi ya Tony Blair, Frank Matsaert alisifu juhudi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuusimamia hadi kuufanikisha mpango huo na kueleza kwamba utakwenda kufungua mafanikio ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kupitia lango la Bandari hiyo.