DC ahimiza stadi za maisha shuleni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:12 AM Sep 27 2024
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James
Picha: Mtandao
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James, amewataka walimu kurejesha somo la stadi za kazi kwa wanafunzi zikiwamo kilimo, mapishi na mambo ambayo yatasaidia kuwaandaa kujitegemea pindi watakapohitimu masomo.

James alitoa agizo akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika wilaya ikiwamo ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari yenye lengo la kuboresha mazingira ya utoaji elimu kwa watoto na kuongeza ufaulu.

Aliwakumbusha walimu wajibu wa kufundisha masomo ya stadi za kazi ikiwamo kilimo kujitambua ili kuwaandaa na maisha ya baadaye kwa kuwa vijana wasiowajibika ni mzigo kwa taifa na jamii kwa jumla.

“Niwapongeze walimu kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kufundisha na kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mitiahani. Lakini niwakumbushe kufundisha darasani pekee haitoshi kuwaandaa watoto kuwa na maisha ya kujitegemea baada ya kuhitimu.

“Kwa hiyo ni muda sasa wa kuanza kufundisha stadi za kazi kama kilimo. Hii  itamfanya mwanafunzi kujitambua na kuwa mtu mzuri, hivyo kuwa na uwezo wa kujitegemea,” alisema.

Kuhusu malezi, James alisema sehemu salama kwa mtoto ni shuleni na kwenye familia kwa hiyo kuna haja kwa walimu kuwa mfano wa kuigwa na wanafunzi nje ya masomo wanayofundisha, ikiwa na maana matendo watakayoyafanya yawe kielelezo kwa wananfunzi wawapo shuleni .

Suala la stadi za kazi linafanya na baadhi ya shule ikiwamo Shule ya Msingi Kalenga ambayo ina mkakati wa kutumia mashamba ya shule kuzalisha mazao. Jamii  imeamua kutumia mashamba hayo kulima mazao kwa ajili ya chakula cha wanafunzi lakini pia yatumike kama shamba darasa kwa wananfunzi kujifunza shughuli za kilimo ili kuwaandaa na maisha ya baadaye.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Shaibu Mingaula, alisema kwa kushirikiana wananchi wa kijiji cha kalenga, wametenga zaidi ya ekari 40 kwa ajili ya kilimo kujihakikishia usalama wa chakula shuleni na kutumia shamba hilo kama shamba darasa la kufudishia watoto stadi za kazi.

“katika kutekeleza azma ya serikali ya kuwapa watoto chakula, kamati ya shule kwa kushirikiana na wazazi, iliamua kuwasilisha wazo kwa serikali ya kijiji ili kuwe na shamba la shule ambalo litahudumiwa na wananchi wenyewe. 

Mpaka sasa  tumefanikiwa kulima kwa msimu mmoja na tunaendelea kujipanga kwa ajili ya msimu wa kilimo ujao. Tumejipanga  kulima mahindi na maharage ili kuwa na uhakika wa chakula shuleni,” alisema.

Baadhi  ya wazazi na wananchi wa kijiji cha Kalenga, wakiwamo Elmina Mgongolwa na Georgina Mhavile, walisema walikubaliana kuwa na shamba la shule ili kupunguza michango ambayo ilikuwa inasababisha watoto ambao wameshindwa kuchangia kutokula chakula wawapo shuleni. 

Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya katika ziara hiyo, alisema mkakati wa halmashauri wa kuhakikisha shule zote zinakuwa na mpango wa chakula shuleni ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na tayari maelekezo yametolewa kwa walimu kusimamia mpango huo.