DART yahamasisha matumizi kadi janja

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 01:22 PM Nov 23 2024
Mkurugenzi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk. Athuman Kihamia akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, wakati akihamasisha wananchi wengi kutumia kadi janja kwenye usafiri mabasi hayo, ili kuwapunguzia usumbufu.
Picha: Joseph Mwendapole
Mkurugenzi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk. Athuman Kihamia akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana, wakati akihamasisha wananchi wengi kutumia kadi janja kwenye usafiri mabasi hayo, ili kuwapunguzia usumbufu.

WAKALA wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), umewataka watumiaji wa usafiri wa mwendokasi kuchangamkia kadi janja ili kupunguza usumbufu wanapotumia usafiri huo.

Mtendaji Mkuu wa DART, Dk. Athuman Kihamia, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza  na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mwitikio wa wananchi katika matumizi ya kadi hizo.

Alisema kadi hizo ambazo zilianza kutumiwa Septemba mwaka huu zilibuniwa baada ya kuona utaratibu wa kutoa fedha taslim kwa wasafiri wanaotumia mabasi hayo ni wa usumbufu.

Utaratibu huo, alisema  ni wa kisasa unaotumiwa maeneo mbalimbali duniani hivyo wananchi wanapaswa kuachana na utaratibu wa kizamani wenye usumbufu na kuhamia kidijitali zaidi.

 “Sasa hivi ukinunua kadi janja kwa Sh. 5,000 unakuta imeshajazwa Sh. 3,000 ambazo unazitumia kwa nauli na uziri wa kadi hii ni kwamba unaweza kuchanja ukiwa kwenye mageti yaliyo njia kuu au ndani ya mabasi,” alisema.

Alisema ili kuhakikisha wananchi wanaotumia usafiri huo wanapata urahisi wa safari yao DART ilinunua kadi 200,000 ambazo zinaendelea kununuliwa na watu wanaotumia usafiri huo na kwamba zimebaki chache.

“Tunashukuru sana kuona mwitikio umekuwa mkubwa watu wamekuwa wakinunua hizi kadi na tunaomba watu waendelee kununua tuondokane na utaratibu wa fedha taslim ambao unausumbufu sana,” alisema.

Dk. Kihamia alisema Septemba, mwaka huu, Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa,  alizindua rasmi kadi janja na mageti janja ambayo yatafungwa kwenye vituo vyote vya mwendokasi.

Alipozindua kadi hizo na mageti, Mchengerwa alisema umefika wakati mwafaka kwa wananchi kutumia kadi janja na kuachana na utaratibu wa tiketi za makaratasi ambao umeshapitwa na wakati.

Pia aliwataka DART  ishirikiane na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kuhakikisha njia ya Mbagala inakuwa na mabasi 500 mpaka kufikia mwezi Desemba mwaka huu kwani njia ya mabasi hayo imeshakamilika.

Alisema hata njia ya Kimara Posta inapaswa kuongezewa mabasi hadi kufikia 170 kwani mabasi yaliyopo sasa hayatoshi na abiria wamekuwa wakilalamika kuchelewa vituoni kwa muda mrefu.

Waziri alisema kama UDART na DART hawawezi kuleta mabasi hayo basi washirikishe sekta binafsi ambayo alisema inauwezo wa kuleta mabasi mengi.