Biteko aipongeza ALAF kwa huduma bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:46 PM Sep 27 2024
Naibu Waziri Mkuu Dk. Dotto Biteko akipata maelezo katika banda la ALAF wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Viwanda (TIMEEXPO 2024).
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu Dk. Dotto Biteko akipata maelezo katika banda la ALAF wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Viwanda (TIMEEXPO 2024).

Naibu Waziri Mkuu Dk. Dotto Biteko ameelezea kuridhishwa na huduma na bidhaa za ALAF Limited Tanzania na kuitaka kampuni hiyo iendelee kuzingatia ubora.

Biteko aliyasema hayo Jumatano wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo katika Maonyesho ya Kimataifa ya Viwanda (TIMEEXPO 2024) aliyoyafungua rasmi katika Viwanja vya Sabasaba.

"Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya na pia Kwa kushiriki katika Maonyesho hata makubwa," alisema.

Biteko pia alihitaji kufahamu ikiwa suala la umeme kiwandani hapo lilishashugulikiwa baada ya kuwepo na malalamiko ya kukatikakatika kwa umeme mara Kwa mara, jambo ambalo lilikuwa linaathiri uzalishaji.

"Mheshimiwa tunakushukuru mno maana suala hili limeshashugulikiwa na sasa uzalishaji unaendelea vizuri,"alijibu Hawa Bayumi ambaye ni Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Alaf.

Meneja huyo aliipongeza serikali kwa kuhakikisha kuwa mazingira ya uzalishaji na biashara kwa ujumla ni mazuri.

"Tunatoa wito kwa serikali iendelee kuboresha mazingira haya zaidi ikiwemo kuangalia sera ambazo sio rafiki kwa wazalishaji na pia kuweka miundombinu sawa ikiwemo barabara ili usafirishaji uwe rahisi," alimueleza Naibu Waziri Mkuu.

Banda la ALAF.
Alieleza kuwa Alaf itaendelea kutoa suluhisho sahihi ya ujenzi kwa ujumla ikiwemo kuja na teknolojia mpya kama inayotumika kujenga maghala ya nafaka Mkoani Ruvuma ambayo imezingatia ubora wa hali ya juu na ni mpya kabisa.

ALAF ni moja ya makampuni yanayoshiriki katika TIMEXPO 2024 yaliyoanza Septemba 26 na yatamalizika Oktoba 2, 2024.

Maonyesho hata yameandaliwa na CTI Kwa kushirikiana na TANTRADE.