KINAMAMA 195 waliokuwa wanasumbuliwa na ugonjwa wa fistula ya uzazi na magonjwa mengine ya wanawake mkoani Lindi, wamepatiwa matibabu bila malipo tangu kuanza kwa ushirikiano kati ya CCBRT, Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi (Sokoine) na Shirika la Equinor Tanzania mwaka 2019.
Tangu kuanzishwa kwa ubia huu, wadau hawa wamekuwa wanaendesha kambi za matibabu ya bure ya fistula mkoani Lindi pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wanaotibiwa na kupona fistula.
Kwa mwaka huu, kambi ya matibabu ya fistula imefanyika tena mkoani Lindi katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi (Sokoine) kuanzia Septemba 9 hadi 13, 2024, ambapo jumla ya wanawake 10 wenye ugonjwa huo mkoani Lindi wamepatiwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hospitali hiyo jana, Meneja wa Miradi wa hospitali ya CCBRT, Yohana Kasawala, alisema "CCBRT inatoa shukrani zake za kwa wadau wake wote, ikiwamo Equinor Tanzania, na kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutushika mkono na hivyo kuwezesha kuwafikia Watanzania wenzetu wenye mahitaji makubwa ya kiafya.
"Kwa mfano, maisha ya wanawake walioathirika na ugonjwa wa fistula yameboreshwa kutokana na matibabu katika Hospitali ya CCBRT na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Lindi - Sokoine."
Alimshukuru Dk. Naomi Makota, Msimamizi wa Miradi ya Jamii kutoka Equinor kwa kushiriki katika kambi inayoendelea mjini Lindi.
Kuhusu mafunzo ya wanawake waliokuwa wanaishi na fistula, Kasawala alisema kuwa mara nyingi wanawake hao hufika hospitalini kwake wakiwa wamekata tamaa na sonona kutokana na kutengwa na jamii zao na wakati mwingine kupoteza wenza na watoto wao.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Upasuaji wa Fistula, Peter Majinge, alisema kuwa hadi kufikia jana, jumla ya wanawake 20 walifika katika Hospitali ya Sokoine na baada ya uchunguzi, wanawake 10 wamegundulika kuwa na fistula ya uzazi, hivyo wanaendelea kupatiwa matibabu ya upasuaji.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dk. Kheri Kagya, aliishukuru CCBRT na wadau wake Equinor kwa kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu wake wa afya ya uzazi mkoani Lindi ili mara baada ya kumalizika kwa mradi huo, waweze kutoa huduma hiyo hospitalini Sokoine kwa kuwa hilo ndilo lengo la mradi tofauti na ilivyo kwa sasa ambapo wagonjwa hulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda CCBRT Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.
Saada Hassan (50) kutoka Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi ni mnufaika wa mradi huo wa matibabu ya fistula. Alikutwa wodini katika Hospitali ya Sokoine, akisema:
"Mwezi uliopita nilisikia tangazo redioni likieleza juu ya ugonjwa huu, baada ya kusikiliza vizuri nilibaini kuwa ndio ugonjwa unaonisumbua, nikachukua namba ya simu waliyotangaza redioni, nikaipiga nikaelekezwa kuwa wataalamu wa matibabu ya fistula toka Dar Salaam watakuwa hapa kwetu Lindi, sikuamini hadi juzi nilipopigiwa simu na kutumiwa nauli ya kuja hospitalini hapa.
"Nimeteseka na fistula ya uzazi kwa takribani miaka 10, baada ya kujifungua mtoto wangu wa mwisho. Kipindi hiki kilikuwa na changamoto kubwa sana, si tu kimaisha bali pia kiroho na kijamii."
Takribani wanawake 3,000 wanaugua ugonjwa wa fistula kila mwaka Tanzania. Wengi wanatengwa na familia pamoja na jamii zao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED