Mil 250 kuendeleza wabunifu Sekta ya Nishati

By Maulid Mmbaga , Nipashe Jumapili
Published at 03:57 PM Sep 08 2024
Mil 250 kuendeleza wabunifu Sekta ya Nishati
Picha: Maulid Mmbaga
Mil 250 kuendeleza wabunifu Sekta ya Nishati

WIZARA ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Umoja wa Ulaya (EU) na Ubalozi wa Ireland, wametoa Sh. Milioni 250 kwa vijana 10 ili kuendeleza bunifu zao zinazolenga kupunguza tatizo la upungufu wa nishati nchini.

Vijana hao 10 wabunifu bora ni sehemu ya 159 waliowasilisha mawazo bunifu na kufanyiwa mchujo na wataalamu waliobobea katika masuala ya nishati, ambako pia walipatiwa vyeti na ruzuku ya Sh. Milioni 25 kila mmoja ili kuendeleza nishati endelevu.
 
Akizungumza leo katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo Naibu Kamishna wa Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Imani Mruma, amesema lengo la kuanzishwa mchakato wa kufadili bunifu hizo ni kuchochea maendeleo ya suluhisho na teknolojia za msingi zenye uwezo wa kuleta athari chanya katika kupunguza matumizi ya nishati.
 
Amesema zaidi ya kuimarisha ushindani wa viwanda, pia ufanisi wa nishati, una jukumu muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Na kwamba hiyo inawiana kwa karibu na Michango ya Kitaifa ya Tanzania (NDC) ya 2021, ambako waliazimia kupunguza utoaji wa hewa chafuzi kwa hadi asilimia 35 ifikapo 2030.
 
“Kutafuta suluhu bunifu zenye ufanisi wa nishati itakuwa muhimu katika kufikia malengo haya kwa kupunguza matumizi, kuboresha usalama wa nishati, na kukuza maendeleo endelevu.
 
“Ubunifu wa ufanisi wa nishati unaweza kuleta mabadiliko katika viwango vyote, ikiwemo katika ngazi ya kaya kwa kusababisha uboreshaji wa matumizi na kuokoa gharama. Pia vifaa vinavyotumia umeme vizuri, teknolojia ya kupikia iliyoboreshwa, na suluhu zilizoboreshwa za kupoza nyumbani, huchangia mazingira bora ya kuishi,” amesema Mhandisi Mruma.
 
Ameongeza kuwa suluhu hizo ni muhimu kwa kuwezesha familia kudhibiti matumizi yao ya nishati kwa ufanisi, na kuimarisha ubora wa maisha yao kwa ujumla. Akieleza kuwa ubunifu huo ni muhimu katika kujenga sekta hiyo na kuiweka Tanzania katika nafasi inayoongoza katika matumizi ya nishati endelevu katika ukanda huu.
 

1

“Kwa washindi, fedha mlizopatiwa zinalenga kusaidia uendelezaji na upanuzi wa ubunifu wenu. Tunawahimiza kutumia fedha hizi ipasavyo ili kuendeleza miradi yenu. Maendeleo yenu yatafuatiliwa kwa bidii, na tumejitolea kuwasaidia katika safari hii yote,” amesema Mhandisi Mruma.
 
Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Muyeye Chambwera, amesema shirika hilo limejitolea kuendeleza ufanisi wa nishati katika nchi zinazoendelea kama vile Tanzania. Na kwamba wanatambua kuwa ufanisi wa nishati si suala la kiufundi tu, bali ni msingi wa maendeleo endelevu.
 
“Tunapojitahidi kufikia malengo ya hali ya hewa ya kimataifa na kukuza ukuaji jumuishi, ufanisi wa nishati unaonekana wazi kama mojawapo ya njia za gharama nafuu na za haraka za kupunguza utoaji wa kaboni, uhaba wa umeme, kuzalisha ajira za kijani, na kuimarisha uwezo wa kiuchumi,” amesema Chambwera.
 
Naye, Naibu Balozi wa Ireland Mags Gaynor, amewapongeza watanzania kwa kuendelea kutoa mawazo mbalimbali ya namna bora ya kufanikisha mradi wa kuwezesha matumizi sahihi ya nishati, na kwamba wataendelea kuunga mkono jitihada hizo ili pia kuwaondolea wanawake changamoto ya nishati safi ya kupikia.
 
“Tunafurahi sana kuona mradi huu unaenda vizuri na niipongeze sana serikali ya Tanzania pamoja na taasisi zake kwa kuendelea kuhakikisha kwamba programu hii inafanikiwa kwa kuleta mabadiliko yatakayochechea maendeleo katika sekta ya nishati,” amesema Balozi Mags.

2