ACT yataja mwarobaini tatizo la ajira

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe Jumapili
Published at 09:07 AM Jul 28 2024
Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu.
Picha:Mpigapicha Wetu
Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema tatizo la ajira kwa vijana kuzunguka na bahasha zenye vyeti hadi zinachakaa kwa ajili ya kusaka ajira, litamalizika iwapo serikali itaongeza nguvu zaidi katika kuwekeza kwenye kilimo na sekta binafsi ambako ndiko kuna ajira nyingi.

Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, alisema hayo jana wakati akiwahutubia wananchi wa Manispaa ya Singida ikiwa ni siku yake ya pili ya ziara mkoani Singida katika kuhamasisha wananchi wakiunge mkono chama hicho ili kufikia lengo la  kuandikisha watu milioni 10 ndani ya miezi 10 ambalo wamejiwekea. 

"Wote tunajua asilimia 61 ya ajira za Watanzania zipo kwenye kilimo. Tulitegemea  angalau serikali ingeona hapa ndipo mahala bora pa kuwekeza na kupata matunda haraka ya watu kuajiriwa. Leo hii kilimo chetu kimegubikwa na changamoto kibao hata bei zenyewe za mazao hazieleweki," alisema. 

Semu, alisema pamoja na kwamba asilimia 25 ya kipato kinatokana na kilimo, katika hali ya kushangaza, kile kinachorudishwa ni kidogo na hii inatoa picha namna ambavyo serikali haijawekeza vya kutosha katika sekta hiyo. 

"Tunashindwa kukitumia sekta ya kilimo kama eneo la kubadilisha maisha ya Watanzania ambao asilimia 61 wanategemea kilimo. Na hatuoni  maofisa ugamvi, wakishughulika na kuongeza  pembejeo za kilimo kwani hazitoshi. Ikumbuke, hivi karibuni kulikuwa na changamoto ya mbolea ya ruzuku ambayo ndiyo tu kwanza imeisha karibuni," alisema. 

Aliongeza kwa kusema kuwa, serikali imeshindwa kuwekeza vya kutosha katika kilimo kwani asilimia 58 ya Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 65 wako kwenye umri wenye nguvu ya kufanya kazi lakini hakuna  mazingira wezeshi ili watu wafanye kazi zitakazowapatia kipato. 

"Singida, nyie mnalima alizeti leo hii bei ya alizeti haieleweki. Inabadilika, leo hivi kesho vile. Wako watu wa katikati wa kutosha alimradi mkulima anazidi kuwa mnyonge badala ya kuneemeka. Badala yake wale watu wa katikati wananufaika na kilimo," alisema. 

Naibu Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo.
Semu, alisema kwa kutambua tatizo la ajira nchini, ACT-Wazalendo katika sera zake itawekeza kwenye kilimo ili kuweza kupata ajira nyingi ambazo zitazalisha kazi kwa ajili ya kuwasaidia vijana nchini. 

"ACT itaweka sera ya kuondoa vikwazo ili kusaidia mtu yeyote anayetaka kuanzisha kiwanda au kuanzisha shughuli ya kupata kipato ili shughuli zisizokuwa na tija ziondoke,"alisema. 

Naye, Naibu Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo, aliwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na siku ya uchaguzi wawachague wagombea kutoka chama hicho ili kuleta mabadiliko. 

Shangwe, alisema katika hospitali ya Mkoa wa Singida, wananchi wanalalamikia huduma mbovu za afya  na kwamba hospitali hiyo haina wahudumu wa afya wa kutosha. 

Naibu Katibu Mwenezi huyo aliwasisitiza wana Singida kuichagua ACT-Wazalendo kwa kuwa ni chama chenye sera bora ya hifadhi ya jamii kwa wote itayokawapa bima Watanzania wote na kutibiwa bila kujali tatizo ni kubwa kiasi gani?

KUBANA MATUMIZI 

Chama hicho pia kimesema kitamaliza tatizo la ajira nchi ili kupunguza umaskini, kuboresha maisha na kukuza maendeleo ya kiuchumi. Katika kufikia azma hiyo, kimesema kutapunguza matumizi ya anasa yanayofanywa na viongozi wa serikali, kuweka vivutio vya kikodi na kuondoa masharti magumu kwa vijana wanaoanza biashara ndogondogo na kufuta sheria zote kandamizi nchini. 

Msimamo huo umeelezwa na viongozi wakuu wa ACT-Wazalendo wakiwa katika majimbo ya Singida Mjini, Muhambwe (Kigoma), Rorya (Mara) na Namtumbo (Ruvuma). Wakiendelea na awamu ya kwanza ya ziara ya kuyafikia majimbo yote 214 ya Tanzania Bara. 

Semu, akiwa jimbo la Singida Mjini alisema ili kuleta heshima na utu lazima vijana wapatiwe fursa za ajira na shughuli za uhakika za kujipatia kipato. Alisema ACT-Wazalendo imejizatiti kupanua soko la ajira na kuhakikisha kila Mtanzania ana shughuli ya uhakika wa kujipatia kipato chake ili kupunguza adha ya vitendo vya uharibifu nchini. 

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita akiwa jimboni Namtumbo alisema iwapo itapewa ridhaa ya kuongoza, ACT-Wazalendo itahakikisha vijana wanaohitimu wanapata ajira kulingana na taaluma zao. 

Alisema msisitizo utawekwa hasa kwenye sekta nyeti zenye upungufu mkubwa wa wataalamu kama vile elimu, afya na kilimo ambao wapo mtaani tu hawajaajiriwa.