Wachezaji Kagera Sugar waahidi kuichapa Azam

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:19 PM Nov 23 2024
Wachezaji Kagera Sugar waahidi kuichapa Azam
Picha: Mtandao
Wachezaji Kagera Sugar waahidi kuichapa Azam

WAKATI wachezaji wa Kagera Sugar wameapa kuondoka na pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Kocha Rachid Taoussi, amesema michezo miwili ya kirafiki waliocheza imesaidia kuwaweka vyema nyota wake ili kupambana kusaka ushindi leo.

Azam itashuka katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuwachapa mabingwa watetezi, Yanga bao 1-0, mechi iliyochezwa Novemba 2, mwaka huu.

Wenyeji Azam wako katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 21 wakati Kagera Sugar itaingia uwanjani ikiwa kwenye nafasi ya 14 baada ya kujikusanyia pointi nane kibindoni.

Joseph Mahundi, mchezaji wa Kagera Sugar, amesema mapumziko ya Kalenda ya Kimataifa yamewafanya kupata muda mrefu wa kupumzika na kujiandaa kikamilifu kuelekea mchezo huo.

Mahundi alisema kwa sasa wachezaji wote wa timu hiyo wana morali na nguvu ya kurejea kwa kasi katika mikiki mikiki ya ligi hiyo, wakianza kuvuna pointi kutoka kwa  Azam FC.

"Baada ya mapumziko ya kupisha michezo ya timu ya taifa, tulirejea kambini na tumefanya maandalizi ya kwenda kuikabili Azam, ni timu kubwa, lakini siku zote tukicheza na Azam panachimbika, mashabiki wataona kesho (leo), nini tutafanya," alisema Mahundi.

Naye Geofrey Manyasi, alikiri wanakwenda kucheza mchezo mgumu, lakini wao kama wachezaji wamejipanga kuhakikisha wanashinda kwa sababu wanataka kutoka chini walipo.

"Sisi kama wachezaji tumejipanga vizuri, tunajua Azam ni timu nzuri, mchezo utakuwa mgumu, lakini kwa jinsi tulivyojiandaa tuna imani tunashinda na kwa bahati nzuri siku hizi timu ikicheza vyema inashinda hata ugenini, hakuna shida yoyote ile," alisema Manyasi.

Taoussi, alisema baada ya Stars kutinga fainali za AFCON, wachezaji wake waliokuwa katika kikosi hicho wamerejea kwa furaha, na morali kubwa, hivyo anaamini itawasaidia pia kwenye mchezo wa leo.

"Tulifanya kazi na wachezaji waliobaki, mbali na wale waliokwenda kwenye michezo ya timu za taifa, tukacheza michezo miwili ya kirafiki ili kujiweka sawa, na hata wachezaji wetu waliokuwa Stars wamerejea, morali yao ingeongezeka kuelekea mchezo huu," alisema Taoussi.