BAADA ya kuwapo kwa sintofahamu ya huenda Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), itaondolewa kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema taarifa hizo si za kweli.
Taifa Stars imefuzu kushiriki AFCON 2025 baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi H ikiwa na pointi 10, nyuma ya vinara Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo), yenye pointi 12.
TFF imesema inashangazwa na taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu uhalali wa mchezaji, Mohammed Ame, ambaye alicheza mechi dhidi ya Guinea, ambayo ilimalizika kwa Stars kupata ushindi wa bao 1-0.
"Tunapenda kuufahamisha umma kuwa Ame ni miongoni mwa wachezaji 23waliokuwa wameorodheshwa kwa ajili ya mechi dhidi ya Guinea.Kabla ya mechi hiyo, wachezaji wa Stars walihaguliwa na timu pinzani pamoja na Kamishna ambapo waliruhusiwa kucheza," ilisema sehemu ya taarifa ya TFF.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, alisema shirikisho hilo halijapokea taarifa yoyote Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuwa ushiriki wa Ame katika mechi hiyo haukuwa halali.
"Taarifa hizo za mitandaoni zisiwazuie Watanzania kuendelea kushangilia ushindi wa Taifa Stars," ilimaliza taarifa ya TFF.
Rais Samia Suluhu Hassan, aliipatia Stars Sh. milioni 700 kufuatia kukata tiketi ya kushiriki Fainali za AFCON zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED