BAO pekee la Leonel Ateba limeipa Simba pointi tatu muhimu mbele ya wenyeji Pamba Jiji FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza jana na kuendelea kukaa kileleni katika msimamo wa ligi hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi 28 baada ya kucheza michezo 11 wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 24 ikicheza mechi moja pungufu huku Singida Black Stars wakishika nafasi ya tatu na pointi 23 kibindoni.
Mechi hiyo iliyokuwa na ushindani kuanzia dakika ya kwanza hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi, Hussein Katanga, ilipolia lakini ni Simba kutoka jijini, Dar es Salaam iliyoenda mapumziko wakiwa mbele na bao hilo lililofungwa kwa penalti na Ateba.
Mshambuliaji huyo kutoka Cameroon alifunga bao hilo na kufikisha goli la tatu msimu huu dakika ya 23 baada ya kuangushwa na beki wa Pamba Jiji ndani ya eneo la hatari na mwamuzi, Katanga kutoka mkoani, Tabora aliamuru pigo la penalti.
Simba walionekana kuutaka ushindi mapema baada ya kuanza kulishambulia lango la Pamba Jiji mapema ambapo dakika ya 17 ya mchezo krosi ya Ladack Chasambi ilimfikia, Chamou Karaboue, lakini shuti lake lilipaa juu.
Pamba Jiji ambao jana walicheza kwa kujituma walionekana kuzidiwa maarifa na wachezaji wa Simba kwa sababu licha ya kupanga mashambulizi hawakufanikiwa kuuvuka ukuta wa Wekundu wa Msimbazi ulioko chini ya Che Malone Fondouh.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Simba walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kufanya mabadiliko baada ya Kocha, Fadlu Davids, kumtoa, Jean Charles Ahoua na nafasi yake kuchukuliwa na Kibu Denis huku pia akiwatoa Debora Fernandes Mavambo, Awesu Awesu na Chasambi na nafasi zao kuchukuliwa na Augustine Okojepha, Omary Omary na Abdulrazaq Hamza ambaye amerejea rasmi uwanjani baada ya kuwa nje zaidi ya mwezi mmoja akiuguza majeraha.
Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo huo licha ya Simba kukosa mabao dakika ya 82 baada ya Kibu kupokea pasi ya Ateba lakini golikipa wa Pamba Jiji, Amos Yona alikuwa makini kwa kuutoa mpira nje na kuzalisha kona tasa.
Kabla ya shambulizi hilo, Pamba Jiji walikosa bao dakika ya 80 baada ya shuti la Samuel Antwi kudakwa kiufundi na kipa wa Simba, Moussa Camara.
Simba inarejea Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravo do Marquis kutoka Angola itakayochezwa Novemba 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa huku wawakilishi wengine wa Tanzania waliobakia kwenye michuano ya CAF, Yanga watashuka dimbani Jumanne kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena leo kwa Azam FC kuikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati KenGold itawaalika Coastal Union na Mashujaa itacheza dhidi ya Namungo FC kwenye uwanja wake wa Lake Tanganyika ulioko mkoani, Kigoma.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED