Watu watano wafariki ajalini Songwe, dereva akimbia

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:58 PM Nov 23 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ( SACP), Augustino Senga.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ( SACP), Augustino Senga.

JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe, limethibitisha kutokea kwa ajali ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu watano, ikihusisha gari lenye namba za usajili T.958 BCS aina ya Scania na bajaji yenye namba MC.783 DUF aina ya TVS.

Kwa mujibu wa  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ( SACP), Augustino Senga, ajali hiyo imetokea Novemba 22, 2024, majira ya saa 3:15 usiku, barabara ya  Mji Mdogo wa Mpemba kuelekea Mji wa Tunduma.

Amesema  bajaji hiyo, ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Emmanuel Hakimu Kalinga, mkazi wa Munganji, Tunduma, ilijaribu kuyapita magari mengine kabla ya kugongana uso kwa uso na gari hilo la Scania.

Amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo ni dereva wa bajaji, Emmanuel Kalinga na abiria , Rehema Sikamnga (25), mfanyabiashara mkazi wa Msongwa, Festo Mambwe (57), mkulima mkazi wa Mbeya, Rosemary Njema (44), mkulima mkazi wa Ipito, Tunduma na Milembe Syiantemi (36), mkulima mkazi wa Kapele.

“Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Tunduma kilichopo Wilaya ya Momba, na tunaendelea na  uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo, dereva wa gari aina ya Scania alikimbia juhudi za kumtafuta zinaendelea,” amesema Kamanda Senga.

Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Senga ametoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanakagua magari yao kabla ya safari na kuzingatia sheria za usalama barabarani wakati wote ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.