Mtoto aliyekatwa koo na dada arejeshewa uwezo kuzungumza

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:14 PM Nov 02 2024
Mtoto aliyekatwa koo na dada arejeshewa uwezo kuzungumza
Picha:Mpigapicha Wetu
Mtoto aliyekatwa koo na dada arejeshewa uwezo kuzungumza

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imemrejeshea uwezo wa kuzungumza mtoto Maliki Hashim (6), ambaye aliupoteza baada ya kupata majeraha shingoni yaliyoathiri koo.

Mtoto huyo, mkazi wa Goba, Dar es Salaam, alikumbwa na madhila hayo baada ya  kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni, Julai, mwaka huu, na anayedaiwa kuwa ‘hausigeli’ wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema mtoto huyo amerejeshewa uwezo wa kuzungumza baada ya kukamilisha matibabu yaliyogharimu Sh. milioni 15 kwa ndani ya miezi minne.

Prof. Janabi alisema matibabu ya mtoto huyo yamefanyika hatua kwa hatua na watalaamu wamejiridhisha kulingana na huduma alizopata.

“Katikati ya Julai, mwaka huu, tulimpokea Maliki hali yake haikuwa nzuri. Kulikuwa na tuhuma dada wa kazi amemkata koo na tulipochunguza, tulibaini alikuwa amekatwa sana koo na lilikuwa karibu linagusa 'voice box' ( kisanduku cha sauti). Hatari  yake ilikuwa angeweza kupoteza sauti maisha yake yote.

“Jitihada ya kwanza iliyofanyika ni kuhakikisha mishipa yote imezibwa ili isiendelee kutoa damu na hatua ya pili ni kisanduku cha sauti kisiathirike na mtoto alikuwa amepoteza fahamu. Alipofikishwa hapa na mama wa Maliki, alikuwa analia muda wote.

“Baada ya upasuaji na siku 25 akiwa ICU (chumba cha uangalizi maalumu) katika saa 48 za kwanza, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema gharama zote tumpelekee yeye na hadi leo (jana) zimefikia Sh. milioni 15,” alisema.

Prof. Janabi alisema baada ya kumtoa ICU kwa siku 25 walimrudisha wodini ambako alikaa wiki mbili na kutokana na madhara makubwa aliyoyapata, walimtengenezea njia ya koo bandia, kwa ajili ya kupumua na kula chakula.

Alisema walimruhusu kurudi nyumbani awamu ya kwanza akisubiri hatua ya pili, ambayo ndiyo hiyo ya kuzungumza.

 “Hatua za kwanza tulifanya na madaktari bingwa wazawa wataalamu wa ENT (sikio, pua na koo). Pia tulishirikisha wenzetu kutoka California, Georgia huko Marekani wamwone, tukamleta mtoto wiki hii na kuingizwa chumba cha upasuaji na leo (jana) tunamruhusu kwa asilimia 100 na hahitaji tena kufanya tiba,” alisema.

Alisema hatua hiyo ya tiba na zingine, inatokana na uwekezaji mkubwa ukiwamo wa vifaa unaosaidia kuleta mafanikio chanya, ambapo nyuma matibabu yake yangefanyika nje ya nchi kwa gharama kubwa.

"Mama na mtoto wangekuwa nje ya nchi kwa miezi minne ni gharama kubwa. MNH tutaendelea kutoa tiba bobezi, uwekezaji huu inawasiadia hata wataalamu tulionao kuonesha uwezo wao,” alisema.

Mbobezi wa Upasuaji Shingo na Mkuu wa Idara ya ENT Muhimbili. Dk. Aslam Nkya, alisema mtoto huyo ameruhusiwa baada ya kujiridhisha amepona tatizo alilopata. Alisema awali alikaa na kifaa cha bandia kooni kwa miezi miwili kuruhusu upumuaji.

"Tumejiridhisha sasa amepona baada ya wiki hii kuangalia kidonda chake kimepona, tumekaa kwa siku mbili na palepokuwa na kovu tumeparekebisha sasa amepona," alisema bingwa huyo.

“Mtoto alipofikishwa hospitalini alikuwa na jeraha mbele ya shingo, lililoharibu tezi la mbele liitwalo (thyroid gland), baada ya kukatwa katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi, kupata maumivu makali sehemu iitwayo (trachea) ambako hewa inatoka kwenye mapafu hupita iweze kwenda kwenye sanduku la sauti, kumwezesha kuhema, kuongea. Kwa hiyo mantiki vyote vimerejeshwa katika hali yake ya kawaida,” alisema.

Mama wa mtoto huyo, Shani Charles, alisema alipofika hospitalini hapo awali, alichanganyikiwa na sasa matibabu yamefanikisha mtoto wake kupona.

Alisema anamshukuru Rais Samia kwa kugharamia tiba na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, ambaye alikuwa na mawasiliano nao mara kadhaa kuhakikisha tiba inafanyika.

“Kipekee ninamshukuru Rais Samia, kwa kulipa gharama za matibabu Sh. milioni. 15. Ninawashukuru watoa huduma wote wa hospitali walioshiriki kumuhudumia mpaka hatua aliyofikia leo kuruhusiwa moja kwa moja, jamii ya Watanzania walioguswa na tukio pamoja na vyombo vya habari vilivyofuatilia kwa karibu jambo hili,” alisema.