Mbowe, Sugu waachiwa kwa dhamana

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:06 PM Nov 23 2024
Mbowe, Sugu waachiwa kwa dhamana

Usiku wa kuamkia leo Mwenyekiti wa Chama cha CHADEMA, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa,Joseph Mbilinyi pamoja na viongozi wengine waliokuwa wanashikiliwa kituo cha Polisi Vwawa wameachiwa kwa dhamana.

Jana mchana, Jeshi la Polisi mkoani Songwe, liliwakamata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, pamoja na vigogo hao kwenye msafara wa kampeni mkoani humo. 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Augustine Senga, alithibitisha kumshikilia Mbowe na makada wengine 11 wa CHADEMA, kwa madai ya kufanya mkutano wa kampeni eneo ambalo hawakupangiwa.

Katika kundi hilo pia yumo Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Songwe, Elia Zambi.

Awali taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema jana zilidai kuwa Mbowe na wenzake walikamatwa na kupelekwa kwenye mapori, hali ambayo iliibua taharuki.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Senga, alisema viongozi na wafuasi hao walikamatwa katika eneo la Lwati, wilayani Mbozi baada ya kufurushwa eneo la Mlowo, walikokuwa wakilazimisha kufanya mkutano kinyume cha ratiba ya wasimamizi wa uchaguzi.

Alisema mbali na kosa hilo, viongozi hao wanadaiwa kufanya vurugu wakati wa ukamataji na kujeruhi askari wawili.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisema jana katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Mbowe alikamatwa baada ya polisi kuvamia msafara wake katika pori la Halungu, lililoko wilayani Mbozi, mkoani humo.

Alisema mkutano wa kwanza ulipangwa kufanyika katika mji wa Mlowo, ulizuiwa na polisi ambao waliwatawanya wananchi kwa mabomu ya machozi. Alisema CHADEMA ilialikwa kwenye mkutano huo ulioandaliwa na ACT-Wazalendo.

“Kabla ya kuwakamata walifuatwa na gari la polisi ambalo lilikutana nao njiani, hivyo liligeuza na baada ya mwendo kidogo walikuta njia imefungwa na magari ya polisi, ndipo walipofungua milango kwa nguvu na kuanza kuwashambulia waliokuwa kwenye magari na kuwakamata kwa nguvu,” alisema Mrema.

Alilitaka Jeshi la Polisi liwaachie viongozi hao bila masharti yoyote ili waendelee na ratiba ya mikutano ya kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.

“Tunalaani kitendo hiki kwani kinaonesha wazi kuwa ni mkakati wa Polisi, kuhujumu kampeni za chama chetu kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Tunaialika Jumuiya ya Kimataifa, kuja kushuhudia uvunjifu wa haki za kidemokrasia kwa vyama vya upinzani nchini katika uchaguzi huu unaoendelea,” alisema Mrema.

Hata hivyo, alisema Mbowe alikamatwa akiwa amefanya mikutano ya kampeni katika Kata ya Itaka, Kijiji cha Itewe na Kata ya Halungu Mjini.

Kwa mujibu wa Mrema, viongozi wengine waliokamatwa ni Mwenyekiti CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi, mbunge mstaafu wa Mbozi Mashariki, Pascal Haonga, Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Wilaya ya Mbozi na Mkuu wa kitengo cha digitali cha CHADEMA, Appolinary Boniface na Mwenyekiti wa chama hicho, Wilaya ya Mbozi, Michael Msongole.

Wengine ni maofisa habari CHADEMA Kanda ya Nyasa, Paul Joseph na Calvin Ndabila, mwanaharakati na kada wa chama hicho, Mdude Nyagali na wasaidizi watatu wa Mbowe ambao ni Adamu Kasekwa (35), Halfan Mbire (37) na Mohammed Ling'wanya, wanaodaiwa kukutwa na visu ambazo ni silaha zisizoruhusiwa kuwepo kwenye mikutano ya kisiasa.

CHADEMA NYASA

Katibu wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Grace Shio, alipinga sababu zilizotolewa na  polisi kuhusu kukamatwa kwa viongozi wao, akidai kuwa ukamataji uliofanywa si halali.

Alisema viongozi hao walikamatwa wakiwa wanarejea katika mkutano wa kampeni katika kijiji cha Itewe, hivyo hakuna kiongozi aliyefanya mkutano katika eneo ambalo halikupangwa.

“Wakati viongozi wetu wanarudi wakiwa katika kijiji cha Halungu, walikutana na gari la OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya)  ya Mbozi, lakini wakiwa wanaendelea na safari ghafla mbele walikuta magari likiwamo la Halmashauri (limetambuliwa) yakiwa yamefunga njia na kuzuia msafara kisha askari kuanza kuwakamata viongozi wetu,” alisema Shio.

Alisema kwa mujibu wa ratiba, chama hicho kilikuwa kifanye mikitano yake katika majimbo mawili mkoani Songwe ambayo ni Mbozi na Tunduma.

"Wametuharibia mikutano yetu mikubwa ya Vwawa na Tunduma, hivyo tunaomba jeshi la polisi liwaachie bila masharti,” alisema.

CCM: TUTAHESHIMU RATIBA

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitaheshimu ratiba zote za kampeni zilizowekwa na kuwaomba viongozi wa watendaji wake, waoneshe hilo katika maeneo yote.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, aliyasema hayo jana katika Kata ya Vingunguti, Jimbo la Segerea, Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya tatu tangu kuanza kwa kampeni za Serikali za Mitaa.

Makalla ambaye ni mlezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, alisema mbali ya kufanya kampeni za kistaarabu, CCM kama chama kiongozi kitaheshimu ratiba zote za kampeni zilizowekwa.

“Niwaombe viongozi na watendaji muoneshe hilo kwa sababu leo (jana), asubuhi kule Songwe kuna chama fulani sintokitaja, kimekurupuka, kulikuwa na katiba ya Chama cha ACT Wazalendo, lakini wao wanataka kufanya mkutano kukatokea sintofahamu.”

“Sisi hatutakuwa kama wale wanaovamia na kushindwa kuheshimu ratiba za kampeni, sisi tutaheshimu,” alisisitiza.

Makalla alisema hawatatumia ukubwa wa chama chao kuvunja taratibu na ratiba za kampeni.

Alisema mpaka wanafika hatua hiyo ya kampeni wamepitia michakato mbalimbali na kusisitiza kwamba, ahadi ya CCM ni kufanya kampeni za kistaarabu na kutumia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, aliwaeleza wana CCM kupiga kura ya ndio hata kwenye maeneo ambayo wako.

Alisema CCM ndio chama cha matumaini na kinachoaminika na kuwataka wapinzani waliko wajiunge CCM na kwamba maandamano yaliyofanyika nchi nzima yaliwanufaisha viongozi na si waandamanaji.

“Leo (jana) mwenyekiti kajikakamua na ratiba yake nimeiona ninawasubiri jukwaani CCM haina utani tumejipanga mitaa yote inakwenda chama tawala,” alisema.

Aliwataka mabalozi, kamati za tawi, za kampeni za kata, za siasa wilaya na mkoa wahakikishe wenyeviti wa CCM ndio wanashinda.

Imeandikwa na Restuta James na Romana Mallya (Dar), Moses Ng’wat, Songwe.