Ajali Fuso yaua wanne na kujeruhi sita

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:17 PM Nov 23 2024
Ajali Fuso yaua wanne na kujeruhi sita
Picha: Mtandao
Ajali Fuso yaua wanne na kujeruhi sita

WATU wanne wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya lori aina ya Mitsubishi Fuso lililokuwa limebeba mawe, kuacha njia na kuparamia wananchi na wafanyabiashara katika eneo la Mataa Bunda Mjini, mkoani Mara.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Mrakibu Msaidizi Augustine Magere, alithibitisha jana kutokea kwa ajali hiyo kwa njia ya simu na kusema alipokea taarifa ya tukio hilo majira ya saa 5:40 asubuhi.

Alisema alipokea taarifa hizo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Vicent Naano, kuwa kuna ajali katika maeneo ya mzunguko Bunda, eneo la barabara iendayo Ukerewe akimtaka kutuma askari kwa ajili ya shughuli za ukoaji.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kuwa katika eneo hilo kuna shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo gereji, ambako tulitaarifiwa kuwa gari liliacha njia na kuparamia jengo hilo wakati watu wakiendelea na shughuli zao za kawaida,” alisema Magere.

Pia alisema alituma kikosi cha askari 10 kwenda eneo la tukio na kuwa mpaka wakati huo alikuwa hajathibitishiwa juu ya majeruhi na vifo katika tukio hilo.

 “Kwa sasa bado hatujawa na taarifa kamili kwani bado shughuli ya uokozi inaendelea, katika jengo hilo lakini taarifa kamili tutazipata baada ya askari wetu kukamilisha shughuli hiyo kukamilika tutaweza kuthibitisha,” alisema Magere.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Dk. Steven Wambura, alithibitisha kwamba watu wanne walikuwa wamefariki dunia huku majeruhi wakiwa ni sita ambao bado wanaendelea na matibabu.